Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga yazikoroga kamati TFF

5th April 2012
Print
Comments
  Papic ajivua lawama kwa Cannavaro
Nadir Haroub `Cannavaro`

Wakati jana jioni Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliendelea na kikao chake cha kujadili rufaa iliyowasilishwa na Yanga kupinga kifungo kwa wachezaji wao watano, kamati hiyo inaonekana kutofautiana na Kamati ya Ligi ambayo nayo imeundwa na shirikisho hilo hivi karibuni.

Katika kuonyesha kwamba kila moja ina majukumu yake, wajumbe wa Kamati ya Ligi walipoitikia wito katika kikao cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kilichofanyika juzi, walikataa kuhojiwa na kueleza kwamba kamati yao iko huru na wao hawakuwa walalamikaji kwenye rufaa inayojadiliwa na kamati ya nidhamu na usuluhishi inayoongozwa na kamanda mstaafu wa polisi katika kanda maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa kamati ya ligi iliwataka akina Tibaigana kushughulikia rufaa iliyowasilishwa mbele yao na kwamba, hawastahili kuwahoji wao kwa sababu nao walitoa adhabu ya kuwafungia wachezaji wa Yanga kama kanuni za ligi zinavyoelekeza.

Baada ya wajumbe hao kuondoka, kikao hicho cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kiliendelea ambapo viongozi wa Yanga walihojiwa kuhusiana na utetezi waliouandaa. Hata hivyo, kikao hicho hakikufikia tamati baada ya kuona taarifa na vielelezo walivyonavyo havikuwa vimekamilika.

Awali, mgongano wa kamati ya ligi ya TFF na kamati ya nidhamu na usuluhishi ulijidhihirisha wakati makamu mwenyekiti wa kamati ya ligi, Said Mohamed alipotishia kujiuzulu na kutaka waombwe radhi na Tibaigana aliyedaiwa kuiita kamati yao kuwa ni ya kisiasa.

Hata hivyo, Mohamed alisitisha kujiuzulu baada ya kukataliwa na rais wa TFF.

 

MSIMAMO WA YANGA

Hadi jana mchana kabla ya kuendelea kwa kikao cha Kamati ya Tibaigana, uongozi wa Yanga ulikuwa unaamini kwamba rufaa yao itashinda na maamuzi ya kuwafungia wachezaji wao yatatenguliwa huku pia yakipunguzwa kwa baadhi ya wachezaji.

Kiongozi mmoja wa Yanga (jina tunalo) alisema kwamba baada ya kushinda rufaa hiyo, ndipo pointi zao tatu ambazo kamati ya ligi iliwapokonya kwa kumchezesha, Nadir Haroub 'Cannavaro' katika mechi yao dhidi ya Coastal zitarejeshwa kwa sababu wanaamini kuwa kadi aliyopewa itafutwa.

PAPIC AJIVUA LAWAMA

Katika hatua nyingine, kocha wa Yanga, Kostadin Papic, aliliambia gazeti hili kuwa lawama za timu yao kupokonywa pointi tatu na kupewa wapinzani wao Coastal Union hazimuhusu kwa sababu alielezwa na viongozi wake kwamba anaweza kumtumia Cannavaro.

Papic alisema kwamba alihakikishiwa na viongozi wa mabingwa hao watetezi kuwa adhabu ambazo zilitolewa na kamati ya ligi zimesimamishwa, hivyo baada ya kukaa nje katika mechi mbili, beki huyo angeweza kumtumia hadi maamuzi mengine yatakapotolewa.

Aliongeza pia jambo la kuwepo kwa adhabu hizo na kusimamishwa naye limemvurugia programu yake aliyoiandaa na kusisitiza kwamba yeye pia hakufurahishwa na vurugu zilizotokea uwanjani wakati wakicheza dhidi ya Azam.

"Mara adhabu ipo, mara adhabu imesimamishwa, hii inanichanganya na sijawahi kuiona katika nchi nyingine nilizowahi kufundisha," alisema Papic.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment