


.jpg)
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema linajukumu la kulipa fidia wakazi wa Ubungo Kisiwani pekee na si kuwatafutia wafanyabiashara ndogo ndogo maeneo ya kufanyiabiashara kufuatia bomoa bomoa ya vibanda vyao vya biashara eneo hilo la mitambo ya umeme.
Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando, alisema suala la kuwatafutia wafanyabiashara hao eneo mbadala si la kwao.
Akifafanua, alisema kwa kufanya hivyo ni sawa na mtu amfukuze mfanyabiashara kwenye eneo lake tena amtafutie eneo la kwenda jambo ambalo halitawezekana.
Akitoa ufafanuzi juu ya malipo ya fidia kwa wakazi wa Ubungo Kisiwani ambapo serikali iliahidi kuwapa fidia wakazi wa eneo hilo kwa kuwa ni hatari kutokana na mitambao ya umeme, Mhando, alisema madai ya wakazi hao ni ya siku nyingi na kwa sasa wanafanya tathimini upya kutokana gharama za vitu kupanda.
“Madai yao ni ya siku nyingi tunachokifanya sasa ni kufanya tathimini kwa malipo ya sasa tutakapomaliza basi tutatoa taarifa kwenu,” alisema Mhando.
Kauli hiyo ya Shirikia la Umeme imetolewa baada ya Mbunge wa Ubungo John Mnyika kutoa siku tatu kwa shirika hilo kuwajibu wananchi wa Kisiwani juu ya malipo ya fidia tangu serikali ilopotangaza toka mwaka 2004.
Hata hivyo, katika mkutano waliyoufanya katika ofisi za kata ya Ubungo aliwaeleza wazi wafanyabiashara ndogo ndogo kuwa haungi mkono biashara kufanyika katika maeneo hayo kwa kuwa ni hatarishi.