



Rais Jakaya Kikwete ametoa orodha ya wajumbe wa tume ya kukusanya maoni kuhusu muundo wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo licha ya kuanza kulalamikiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kuhusu kiwango au wingi wa uwakilishi wao, ni nzuri.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba siyo jopo la kisiasa la kuendesha mjadala bali tume ya kufanya maamuzi ya nini kinachofaa katika nchi. Kwa upande wa JK suala halikuwa mizania ya wawakilishi wa vyama vya siasa bali makundi ya jamii. Hapo ndipo utaalamu au usanifu wa kuchagua wajumbe wa tume unapoonekana, kuwa hakuna kundi lililoachwa nje.
Ulalamishi kuhusu kiwango cha uwakilishi wa vyama vya upinzani unafanya kosa la kiufundi la awali, la kudhania kuwa huo ndiyo msingi halisi wa kuteua wajumbe – suala walilokuwa wakilihofia tangu mwanzo.
Ni kweli kuwa vyama vipo katika tume hiyo lakini havikuingizwa kama vyama ila kwa sababu miongoni mwao wako wataalamu wasiopingika uwezo wao wa kuchangia kufafanua mantiki ya hili au lile katika kukusanya na kujadili hoja za katiba gani inahitajiwa. Wamechaguliwa katika tume kwa ajili hiyo na kwa njia hiyo kama wataalamu, si kama wawakilishi wa vyama kwani sifa hiyo ni hasi kwa tume.
Ina maana kuwa itikadi ya kushiriki katika kazi ya tume ni kutanguliza utaalamu, na siyo itikadi kwani kama kila mjumbe atakuja na itikadi maalum ambayo watu wake wamemwambia wanataka idhihirike katika kazi ya tume au maamuzi yake, mkwamo utafuata.
Ila kama watatanguliza utaalamu wao, pale anapokazania mtu mwelekeo fulani au muundo na wazo hilo halipendezi kwa wengine, atasahihishwa kitaaluma na suala litaishia hapo. “Wakiumana” katika utaalamu wa suala fulani, tume hiyo ambayo inaongozwa na majaji wazoefu, Joseph Sinde Warioba na Augustino Ramadhani, itafuata mwenendo wa mahakama, yaani uamuzi unatolewa kuhusu utata wa kisheria uliojitokeza, na hapatakuwa na ubishi.
Ina maana pia kuwa kuna kazi ya kurekebisha hisia na matazamo kwa upande wa jamii, kuwa makundi tofauti ya jamii yasianze kutoa matamshi-jumla ya mwelekeo wa kuunda katiba mpya na kutazama kuwa wale walioingia kwenye tume watayatetea.
Badala yake, wanatakiwa watoe mawazo kama hayo iwe ni kwa ushiriki katika kazi ya tume inapokutana na wananchi, au kwa kupeleka hoja hizo na kuzieleza kwa kina kwa mmojawapo kati ya wajumbe ili aziwakilishe na kuzitetea.
Ina maana kuwa pale wajumbe wa tume watakapofikia uamuzi kuhusu suala hilo, makundi yamsikilize mjumbe waliye karibu naye, si kupaza sauti na kudai kuwa ‘kama hili halifanyiki basi hapatakalika,’ kwani mwelekeo huo haujengi nchi.
Ni wazi kuwa tume hiyo itafanya kazi yake kitaaluma na kwa kuzingatia hisia za makundi tofauti ya jamii katika maskani yao na shughuli zao, masuala ambayo ni ya msingi zaidi kuliko yanayotajwa na wachache kati yao ambao wanakuwa katika mstari wa mbele kwenye vyama vya siasa.
Makundi hayo ya kisiasa ni ziada tu ya makundi ya msingi zaidi katika jamii ambayo hasa ni maeneo ya kuzalishwa, kazi na uhusiano wake na vyombo vya nchi katika kazi hizo (kwa mfano wafanyabiashara, walemavu, wanasheria, wasomi wa vyuo, n.k,) Alichokifanya JK ni kulenga makundi halisi ya jamii, na siyo yale ya ushabiki tu wa kisiasa.
Kwa maana hiyo utaalamu na uwakilishi wa tume hauna mjadala, na kilichobaki ni itikadi miongoni mwa wajumbe wake wanapoanza kazi. Vyama vya siasa vinaweza kutofautiana makundi ya jamii hayawezi, lazima waishi pamoja ili kila mmoja awe salama. Wajumbe wakikumbuka ulazima huo, wataafikiana.
Mungu ibariki tume yetu, Mungu Ibariki Tanzania.