Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tujipange sawa sawa kukabiliana na majanga

12th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Majanga mengi yanayotokea nchini, kama ya mioto, mafuriko na hata ajali za magari yanathibitisha kwamba uelewa wa watu wetu kwa ujumla juu ya kinga ya matukio kama hayo ni mdogo sana na hata pale janga linapotokea, basi njia za kukabiliana nalo imekuwa si yenye ufanisi wa kutosha kiasi cha kusaidia ama kuokoa maisha au mali.

Juzi jijini Arusha baa ya Pentagon na nyumba moja yenye maduka manane viliungua na kutekekea kabisa kwa moto uliozuka, ingawa habari njema zilieleza kuwa hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu.
 
Tukio la Arusha linatokea siku chache tu baada ya janga jingine la moto kutokea katika soko kuu la samaki la Feri lilikoko jijini Dar es Salaam, moto mkubwa uliunguza sehemu ya paa la soko hilo sehemu ambayo samaki hukaangwa na wachuuzi. Hili la soko la Feri ni tukio la tatu kutokea, na madhara yake kwa uharibifu wa mali umekuwa ni mkubwa sana.

Kama ilivyotokea kwa tukio la juzi la Arusha, kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Arusha, kilipata wakati mgumu kuuzima moto huo uliotokea mtaa wa Chini ya Mti karibu na barabara ya Chagga, mkabala na ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Auwsa).
 
Moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika, ulizuka kuanzia saa 5:00 asubuhi na juhudi za kikosi hicho za kuuzima hazikufanikiwa mara moja, kwanza kutokana na kutokuwa na maji ya kutosha kwa maana ya kuishiwa maji na kukosa sehemu ya kujaza gari lao kwa haraka, pili ukosa tu ufanisi wa kufanya kazi hiyo kiueledi.

Hali hii iliwafanya wananchi kutumia zana duni, kama mchanga, ndoo za maji na wengine kudiriki kupanda juu ya mapaa ya nyumba hizo na kuengua mabati na mbao ili kunusuru baadhi ya nyumba zisishike moto uliokuwa unawaka kwa kasi kubwa.
 
Inawezekana kabisa ubovu au udhaifu wa miundombinu ya kukabiliana na majanga ya moto ni chanzo kikuu cha kusindwa kwa kikosi cha zima moto kokote kiliko nchini, kwani kila wanapofika kwenye eneo la tukio, ama huishiwa maji mara baada ya kutumia yale waliokuwa nayo au hujikuta vifaa vyao vikikosa ubora na umadhubutu wa kuhimili kazi ya kuzima moto.

Kwa mfano, kuna tukio la kikosi hicho kufika eneo la tukio lakini mipira yao ya maji ilikuwa imejaa matundu kiasi cha kushindwa kurusha maji kwa presha inayotakiwa kuufikia moto.

Haya yakikumba kikosi cha zima moto, vikosi vya binafsi vya zima moto na uokoaji, kama Knight Support, vimekuwa vikifanya kazi, na hata katika tukio la Arusha kilifanya kazi nzuri. Hali hii inaacha swali moja, hivi ni kwa nini kikosi cha zima moto na ukoaji cha umma kimetelekezwa hivi, kwa maana ya kunyimwa zana, mafunzo na hata kukosekana kwa utayari wa kutekeleza majukumu yake.

Kwa wale waliopata fursa ya kutembelea nchi za wenzetu waliopiga hatua za maendeleo, hakika utagundua kitu kimoja, hawana mzaha hata kidogo na majanga yawe ya asili au yanayotokana na shughuli za binadamu. Saa zote wamejiandaa kukabiliana nayo. Ishara na vielelezo vya aina mbalimbali vimewekwa wazi juu ya kukabiliana na majanga hayo, mafunzo hutolewa kila wakati kuhakikisha kuwa kila raia anajua cha kufanya mara majanga hayo yatokeapo.

Hawaishii kutoa elimu tu, vifaa vya ukoaji vimewekwa wazi, mathalan, shemu za kujaza maji magari ya zima moto ili kutimiza majukumu yao yameweka kila kona, nia ni kurahisisha kazi hiyo. Kikubwa zaidi, utayari wa kukabiliana na majanga haya ni kitu kinachopewa umuhimu wa hali ya juu mno.

Hapa kwetu ukiacha viwanja vya ndege ambako pengine ni kwa sababu ya kuwako kwa sheria za kimataifa za kulazimisha uwepo wa vikosi vya zima moto na ukoaji kwa usalama wa ndege na abiria, maeneo mengine yote suala la utayari wa kukabiliana na majanga ya moto ni kama halipewi umuhimu wowote wa maana.

Ukitazama jinsi ujenzi wa majumba makubwa makubwa kama yaliyotanda eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam kwa sasa, hakika utagundua kuwa uelewa wa watu wetu, na umakini wa vyombo vya usimamizi kuhusu kukabiliana na majanga, si suala linalotazamwa kama la umuhimu kwa usalama wa maisha na mali, bali ni aina nyingine tu ya kero.

Kwa hali hii wengi hawazingatii na vyombo vya usimamizi navyo havijali kwa kuhakikisha sheria za usalama katika kukabiliana na majanga haya zinafuatwa vilivyo. Sisi tunasema sasa ni wakati wa kubadilika ili kudhibiti majanga haya.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment