


Wagombea 33 kwenye Bunge la Afrika Mashariki wameteuliwa kuwania nafasi hiyo huku mgombea mmoja akienguliwa baada ya kushindwa kukidhi vigezo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ilisema wagombea hao wanatoka vyama vya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na TADEA.
Dk. Kashililah alisema wagombea hao walirejesha fomu hizo katika ofisi za Bunge kabla ya saa 10.00 jioni Aprili 10 mwaka huu.
Alisema mgombea ambaye alishindwa kukidhi vigezo vya kuwania nafasi hizo tisa, ni mgombea kutoka chama cha CUF, Mohamed Dedes.
Alisema Dedes alishindwa kuthibitisha uraia wake na kulipa ada ya uchaguzi kwa mujibu wa kanuni ya 5(3), na 6 ya nyongeza ya tatu ya Kanuni ya Bunge na hivyo hakuteuliwa.
Aliwataja wagombea waliopitishwa kuwania uchaguzi huo utakaofanyika Jumanne ya wiki ijayo (17/4/2012), katika kundi la wanawake ni Angela Kizigha, Fancy Nkuhi, Dk. Godberth Kinyondo, Janet Mmari, Janet Mbene, Maryam Yahya, Sebtuu Nassor, Shy-Rose Bhanji na Sofia Rijaal wote kutoka chama cha CCM.
Wagombea kutoka Zanzibar ambao wote kutoka CCM ni Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Dk. Ahmada Hamad Khatib, Dk. Haji Mwita Haji, Khamis Jabir Makeme, Dk Said Gharib Billal na Zubeir Ali Maulid.
Wagombea kutoka vyama vya upinzani ni Antony Komu( Chadema) , Twaha Taslima(CUF) na Micah Mrindoko (TLP), Dk. Fortunatus Masha (UDP) , John Chipaka (Tadea), Juju Danda, Mwaiseje Polisya, Nderakindo Kessy wote kutoka NCCR-Mageuzi. Alimtaja Rose Mwalusamba pekee ndiye anayetoka kambi ya upinzani ambaye anagombea kwa tiketi ya Chama cha CUF.
Wagombea katika kundi la wanaume kutoka Bara ni Adam Kimbisa, Bernard Murunya, Charles Nyerere, Dk. Edmund Mndolwa, Elinariki Kingu, Dk Evans Rweikiza, Mrisho Gambo, Siraju Kaboyonga na William Malecela.
Naye Katibu wa wabunge wa Chadema, John Mnyika, alitaka kurekebishwa kanuni za uchaguzi huo ili kuhakikisha uteuzi na uchaguzi unakuwa huru na haki kuepusha kasoro zilizojitokeza mwaka 2006 wakati wa Bunge la tisa.
Alisema kufuatia tatizo hilo, amemwandikia barua Spika na katibu wa Bunge kumuomba wachukue hatua za haraka kurekebisha mchakato wa uchaguzi husika ikiwemo kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya Kanuni kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili.
Alisema kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, chama kimoja kinatarajiwa kuwa na nafasi nane miongoni mwa nafasi tisa za wabunge wa Afrika Mashariki.
Mnyika alisema kuwa kulingana na uwiano wa idadi ya wabunge bungeni, CCM ilitakiwa kuwa na wabunge saba katika uchaguzi huo, Chadema mmoja na CUF mmoja.