


.jpg)
Mshambiliaji wa timu ya soka ya vijana ya taifa ya umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Thomas Ulimwengu, juzi alishindwa kujiunga na wenzake kama ilivyotarajiwa kutokana na kuchelewa ndege kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako ndiko anaichezea klabu ya TP Mazembe imefahamika.
Ulimwengu ndiye yosso pekee kutoka nje ya nchi ambaye ameitwa na Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Kim Poulsen, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali zijazo za vijana za Afrika dhidi ya Sudan utakaofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na NIPASHE, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Ulimwengu alichelewa ndege na hivyo mambo yakienda vizuri yosso huyo alitarajiwa kuwasili nchini jana usiku.
Wambura alisema kwamba tayari mchezaji huyo alisharuhusiwa na klabu yake kuja kujiunga na timu hiyo ya vijana hivyo hakuna kikwazo kutoka kwa klabu yake.
"Tunamtarajia awasili leo (jana) saa 2 usiku, jana (juzi) alichelewa ndege Lubumbashi," Wambura alisema kwa kifupi.
Wambura alisema pia bado taarifa za ujio wa yosso hao wa Sudan haijajulikana lakini akaongeza kuwa maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri.
Habari zaidi kutoka kwenye kambi ya timu hiyo zinaeleza kwamba wachezaji wengine kutoka klabu ya Mtibwa Sugar, nao walichelewa kuripoti kambini jambo ambalo linamuweka Kim kwenye wakati mgumu wa kutekeleza programu zake.
Kim ambaye aliletwa kwa mapendekezo ya kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen, aliiongoza vyema timu hiyo mwaka jana ilipokuwa imealikwa kwenye mashindano ya COSAFA ambapo ilimaliza hatua ya makundi ikiwa ya pili.
Yosso hao wa Tanzania na Sudan watarejeana jijini Khartoum baada ya wiki mbili ambapo mshindi atakutana na timu ya vijana ya Nigeria baadaye mwezi ujao.