Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

`Mafisango alikuwa mcheshi, alitutafsiria kiarabu`

18th May 2012
Print
Comments
Picha ya gari la Patrick Mafisango lilivyo kufuatia ajali iliyochukua maisha ya kiungo huyo wa Simba.(Picha zote: Omar Fungo)

Kama vile alikuwa anafahamu kuwa ndio siku zake za mwisho zimefika, kiungo wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango, alikuwa ndiye mchezaji mcheshi na mchekeshaji katika timu hiyo hiyo kuanzia wakati timu hiyo inaondoka na ilipokuwa safarini kurejea jijini Dar es Salaam ikitokeza mjini Shandy, Sudan.

Kiungo huyo wa zamani wa mabingwa wa soka wa Ligi Kuu ya Rwanda, APR na ambaye alikuwa amerejeshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi) alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Keko (kona ya mtaa wa Mbozi) jijini Dar es Salaam.

Mafisango bila ya kufahamu lugha ya kiarabu wakati timu yao ikiwa kwenye ndege ikirejea jijini alikuwa akitafsiri maneno yaliyokuwa yanazungumzwa kwa lugha hiyo akielezea Simba ilivyofungwa na kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho huku akiwataka wachezaji wenzake waamini na kuyakubali matokeo hayo.

Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, ambaye jana alikuwa ni mmoja wa viongozi waliokuwa wanasimamia taratibu za kufanyiwa uchunguzi na kuhifadhiwa mwili wa marehemu Mafisango.

Daktari huyo ambaye alikaa sana na marehemu Mafisango baada ya Simba kutoka uwanjani ambapo ilikuwa imepoteza mchezo huo wa kimataifa kuwa alisema kuwa ili timu hiyo iweze kufanya vizuri viongozi wasikipangue kikosi cha kwanza.

"Na wachezaji ambao wanapaswa kuongeza ni beki wa kati, kiungo na mshambuliaji," Mafisango alimueleza daktari huyo wa Simba.

Daktari Kapinga alimuelezea kiungo huyo kuwa alikuwa ni mzoefu na mara nyingi uwanjani alionekana kuchukua jukumu la unahodha kwa kuwapa maelekezo wachezaji wenzake ili kuhakikisha timu inapata ushindi.

"Simba imepoteza mpiganaji, alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliokomaa ndani na nje ya uwanja, ni pengo na sijui niseme nini kuhusiana na mchezaji wetu," alimaliza daktari huyo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa mchezaji huyo alikuwa kwenye mipango ya maendeleo ya timu yao na mchango wake ulikuwa unahitajika bado.

Kaburu alisema kuwa wamesikitika kumpoteza nyota huyo hali ya kuwa Simba ilikuwa iko kwenye harakati za kumpa mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo.

"Tumeumia na tunaendelea kuumia, kama siamini lakini yote ni mipango ya Mungu, ni kilio chetu wote," alisema kiongozi huyo.

Kaburu aliongeza kuwa si Simba peke yake, hata Rwanda pia itamkumbuka kwa sababu alikuwa amepokea tiketi ya ndege ya mchezaji huyo ikimtaka aondoke jana kuelekea Kigali kujiunga na kambi ya Amavubi.

Naye Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, aliliambia gazeti hili kuwa juzi alikuwa akimsataka mchezaji huyo kuanzia asubuhi lakini simu yake ilikuwa haipatikani.

Mtawala alisema kuwa alifanikiwa kuongea na marehemu Mafisango juzi saa 3 usiku na kumueleza kwamba jana alitakiwa akutane na viongozi kwa ajili ya kumsainisha mkataba wa mpya wa miaka miwili baada ya kuridhishwa na kiwango chake.

WACHEZAJI WENZAKE
Emmanuel Okwi wa Simba, alilieleza gazeti hili kuwa ameumizwa sana na kifo cha mchezaji huyo na anasema kwake ni pigo kwa sababu alikuwa ni zaidi ya rafiki.

Okwi alisema kuwa mafanikio yake katika soka yamechangiwa na marehemu Mafisango kwa sababu kila mara alikuwa akimkumbusha namna anavyotakiwa kucheza na kujiendeleza kimaisha.

"Jana (juzi) tulipanga ndio tukae pamoja ili tujipongeze kwa kumaliza msimu wa ligi na kutwaa ubingwa, lakini sikuweza kuonana nae, watu wengi walikuwa wakimtafuta akiwemo Micho (Sredojevic Milutin- Kocha Mkuu wa Amavubi) ambaye alinieleza anataka kuzungumza na Mafisango lakini hampati, nimweleze kwamba anatakiwa kwenda Kigali," alisema Okwi huku akilia kwa uchungu.

Okwi aliwataka viongozi, wachezaji na wanachama wa Simba kuhakikisha wanashiriki kuisaidia familia ya mchezaji huyo katika kipindi hiki kigumu na kumuenzi kutokana na mchango wake.

HARUNA NIYONZIMA
Kiungo huyo wa Yanga na Amavubi aliliambia gazeti hili jana kuwa licha ya kuuona mwili wa Mafisango ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti lakini bado haamini kama Simba na Rwanda wamempoteza mchezaji huyo.

Niyonzima alisema kwamba kuondokewa kwa mchezaji huyo ni pengo kwa sasa kutokana na mchango wake ulikuwa bado unahitajika katika kupata ushindi.

"Ni mapema na ghafla sana mwenzetu ameondoka, ni pengo, ila mpaka sasa siamini kilichotokea, Kigali yote inaniuliza juu ya msiba huu," alisema Niyonzima.

Aliongeza kuwa anakumbuka wakati wa mechi ya kufunga ligi kati ya Simba na Yanga, marehemu Mafisango, alikuwa akimueleza kwamba mpira ni kazi na lazima upambane wakati wote.

"Kila nilipokaribiana naye alikuwa akinieleza maneno kwa Kinyarwanda akiniusia na kuniambia mechi ikiisha nibadilishane naye jezi na nisimpe mtu yoyote jezi hiyo kwa sababu ndiyo itakuwa kumbukumbu yangu," Niyonzima alinyamaza na kuanza kulia.

UHURU SELEMANI

"Kwa kweli ni msiba mkubwa kwetu Simba, siamini lakini ndiyo hivyo tena yametokea, nilipita eneo hilo la tukio muda mfupi kabla ya ajali, tutaendelea kumkumbuka daima.

BOBAN AKWEPA PAPARAZZI
Haruna Moshi 'Boban' alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliofika katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kuhakikisha kama kweli aliyoelezwa ni sahihi huku akiwa analia kwa uchungu.

Hata hivyo Boban hakuweza kurejea kupitia njia ya kawaida iliyozoeleka na badala yake alizunguka kupitia mlango wa nyuma wa jengo hilo la kuhifadhia maiti na kuondoka kimya kimya.

Boban ni mmoja kati ya watu wachache waliofanikiwa kuuona mwili wa marehemu Mafisango.

AZAM YAMLILIA MAFISANGO
Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji huyo na watamkumbuka sana kutokana na mchango wake akiwa ndani ya klabu hiyo.

Nassor alisema kuwa kiungo huyo aliyeaga dunia ghafla alikuwa ni mmoja wa wachezaji wanaofaa kuigwa kutokana na kuwa na ushirikiano na wachezaji wengine bila ya kujali chipukizi au ni wakongwe.

"Tumepokea kwa majonzi msiba huu, tulimfahamu na tulivutiwa naye alivyokuwa APR, na yeye ni mmoja wa wachezaji waliochangia mafanikio ya Azam yanayoonekana sasa," aliongeza Nassor.

Marehemu Mafisango alizaliwa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwaka 1980 na kutokana na kiwango chake nchi ya Rwanda ilimpa uraia ili aweze kuichezea timu yao ya taifa.

Kiungo huyo ameacha watoto watatu, mmoja ni Crespo (3) ambaye alikua akiishi naye hapa jijini na mama yake akiwa China kibiashara.

Mungu ailaze Roho ya marehemu mahali pema pepeni, Amen.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment