Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TBS yapata Mkurugenzi mpya

26th May 2012
Print
Comments
Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

Wiki moja baada ya agizo la kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bodi ya Wakurugenzi ya  Shirika hilo imemteua Leandry Kinabo kuwa Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa shirika  hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya TBS, Oliver Mhaiki,  alieleza hayo katika mahojiano na NIPASHE Jumamosi,  juu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdalah Kigoda, kuiagiza Bodi  hiyo kumsimamisha Mkurugenzi wa zamani, Charles Ekelege ili kupisha uchunguzi .Mhaiki alisema Kinabo aliyekuwa Mkurugenzi wa Viwango, alichukua nafasi hiyo baada ya Bodi kumuondoa Ekelege kwenye wadhifa huo mapema  wiki  hii.

Alifahamisha kuwa kikao cha bodi ya shirika hilo kilifanyika jijini Dar es Salaam, Jumatatu  wiki hii  na kutekeleza maagizo ya Waziri Kigoda ya  kumsimamisha kazi  ili kupisha uchunguzi.

Alipoulizwa iwapo uchunguzi wa tuhuma zake umeanza na taasisi zipi zinazomchunguza mtendaji huyo wa zamani wa TBS, Mhaiki hakuwa tayari kuzungumzia  hoja hiyo.

Habari za ndani kutoka TBS zilisema kuwa uamuzi wa kumsimamisha kazi ulikuja siku moja baada  ya Mkurugenzi huyo kurejea nchini akitokea ziarani China na Japan, alikokwenda kwa siku 10.
Zilieleza kuwa alirejea nchini Alhamisi wiki iliyopita  wakati hatua ya kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi ilitangazwa na Waziri Kigoda  Ijumaa iliyopita.

Ekelege alisimamishwa kazi kufuatia tuhuma dhidi yake zilizoibuliwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), kuwa TBS  ililidanganya taifa kuwa ina wakala wa kukagua  na kukusanya mapato ya magari yanayoingizwa nchini kutoka  katika mataifa ya Hong Kong na Singapore.

Wakala huyo alidaiwa kuwa ana wafanyakazi , ofisi na  anafanya shughuli za uendeshaji  kila siku.  Wajumbe wa POAC  waliozuru mataifa hayo kuona shughuli za wakala huyo  ‘hewa’  baada ya kuugundua ukweli walipendekeza Mkaguzi na Mdhibiti  Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Mapato TRA kukagua na kukadiria hasara iliyopatikana kufuatia udanganyifu huo.

Kashfa  ya TBS ni miongoni mwa sababu zilizosababisha Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami, kuondolewa katika wadhifa huo katika mabadiliko ya kulisuka upya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles