Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Pongezi TASWA kutoangalia rangi

9th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo(TASWA)jana kilitangaza orodha ya wanamichezo wanaowania tuzo mbalimbali za fani hiyo kwa mwaka uliopita wa 2011.

Patakuwa na tuzo za michezo mbaimbali usiku wa Alhamisi,siku ambayo chama hicho kitafanya hafla ya kutunuku wachezaji hao ambapo washindi wa kila kipengele cha mchezo mmoja watashindana ili kumpata Mwanamichezo Bora wa Mwaka jana.

Lakini katika mchezo unaopendwa na watu wengi zaidi duniani, soka, na ambao ndiyo wenye kuteka zaidi hisia za wapenzi wapend michezo TASWA imefanya jambo ambalo sisi, Nipashe, hatukulitarajia.

Katika nchi ambayo kuna utani kuwa mtoto huzaliwa akiwa tayari amesajili kuwa shabiki wa Yanga ama Simba,hapakuwa na jina la mchezaji wa Jangwani katika orodha ya TASWA ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka.

TASWA imewataja Juma Kaseja wa Simba, na Aggrey Moris na John Bocco kutoka Azam kuwania tuzo hiyo.

Tunafahamu, Nipashe, kwamba msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Yanga ambayo si tu ilishika nafasi ya tatu kwenye ligi, ya chini zaidi, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1988 lakini pia ilichezea kichapo chake kikubwa zaidi kutoka kwa timu ya nyumbani kwa karibu miaka 40, kutoka kwa Simba cha 5-0.

Lakini pamoja na kuwa na 'mwaka wa shetani' huo bado palikuwa na uwezekano kwa TASWA kutoka na orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka yenye jina la 'kifaa' cha Yanga kutokana na baadhi ya wajumbe wa kamati yake ya maandalizi kuwa, kwa vyovyote, walizaliwa wakiwa wameshasajiliwa kuwa mashabiki wa Yanga.

Si siri. Msimu wa Yanga, na hivyo mwaka 2011 ulikuwa mbaya kwa klabu hiyo iliyotumia muda mrefu kushughulikia migogoro kwanza, uliomtoa makamu mwenyekiti DAvis Mosha na baadaye mwenyekiti mwenyewe Lloyd Nchunga madarakani.

Kwasababu kinachowekezwa kwenye klabu ndicho ambacho hujidhihirisha uwanjani, kiwango cha wachezaji wa Yanga msimu uliopita kiliendana sambamba na matokeo yake ndani ya uwanja hivyo kujikuta ikikosa ushiriki wa michuano ya klabu ya Afrika mwakani.

Na katika ligi ambayo mafanikio huangukia kwa timu mbili tu za kwanza, kwa kushika nafasi ya tatu Yanga ilitoa mwanya kwa TASWA kuwa na uwezo wa kuweka mbali ushabiki wa timu miongoni mwa wajumbe wake na kuwatosa wachezaji wa klabu hiyo kongwe.

Panaweza kujitokeza malalamiko kutoka kwa mashabiki waliokubuhu wa Yanga kwamba timu yao imeonewa.

Lakini TASWA itaweza kurejea hata uteuzi wa timu ya taifa kama vigezo vya kiufundi vilivyozingatiwa katika mchakato huo vitakuwa vigumu kueleweka kwa wapenzi wa Jangwani.

Katika kikosi chake cha kwanza cha timu ya taifa, Taifa Stars, cha wachezaji 23 kocha mpya Mdenmark Kim Poulsen aliita mchezaji mmoja tu wa Yanga.

Mgeni huyu naye alipendelea?
Wakati tukitafakari ujasiri huu wa TASWA, pengine ni wakati wa kushauri wanachama wa klabu zetu, hasa Simba na Yanga ambazo zinatarajiwa kuwa dira ya maendeleo ya mchezo huo nchini, kufahamu kuwa si tu wakati wa migogoro umepita lakini pia mara zote migogoro hiyo huwa hailipi.
 


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment