



Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, amesema wanawake wa Tanzania wanatakiwa kuungana na kumuomba Mungu ili aiponye nchi na majanga mbalimbali.
Alitoa kauli hiyo, wakati akifunga kongamano la kitaifa la wanawake waombolezao, lililodumu kwa siku tatu katika ukumbi wa Sinza Christian Centre, jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo ambalo liliwajumuisha wanawake 70 kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na Visiwani na wageni 32 kutoka nchi za Zambia, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, Malawi, Uganda, Kenya, na Marekani, lilifunguliwa Juni 7 na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Seif Iddi.
“Tutumie nafasi yetu kama wanawake, kuunda jeshi kubwa la maombezi kwa ajili ya nchi yetu. Nchi hii inahitaji maombi na kwa hakika inamuhitaji Mungu iwe ni kwenye huduma zetu, ndoa zetu, familia zetu na uchumi wetu binafsi na taifa kwa jumla,” alisema.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwaomba akinamama kuwaombea wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi zaidi ya milioni 45 kwani wanatarajiwa kuanza kikao cha Bunge Jumanne ijayo.
“Tumuombe Mungu awaguse waheshimiwa Mawaziri na Wabunge ili wabaini kwamba wana jukumu la kuhakikisha wanafanya maamuzi ambayo yatawasaidia Watanzania kujikwamua kutoka kwenye umaskini na hatimaye waweze kupata maisha bora,” alisema.
Pia aliwataka wakinamama hao kuwaombea Watanzania wawe na uzalendo wa kuipenda na kuithamini nchi yao, wawe na moyo wa kufanya kazi kwa bidiii na siku zote wawe mstari wa mbele kuitakia mema nchi yao.
Mapema, akitoa mada kuhusu ukomavu wa kiroho, Mwalimu Nikku Kyungu kutoka Marekani, alisema wanawake wa Tanzania wana nafasi ya kubadilisha mambo kama tu watampa Mungu nafasi ya kutenda na kuacha kuomba kwa mazoea.
Kongamano hilo liliandaliwa na Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches chini ya uongozi wa Askofu Godfrey Malassy ambaye ni Mwenyekiti wa Mkesha Mkubwa wa Kitaifa.