



Jana Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kupinga ajira kwa watoto. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘Haki za binadamu na haki za kijamii, tutokomeze ajira kwa watoto’ ukiwa ni ujumbe wa kuikumbusha jamii kwa ujumla wake kuwa ajira kwa watoto siyo kitu kinachoungwa mkono, utumikishaji wa watoto ni ukiukaji wa haki za msingi za watoto.
Nchini Tanzania asilimia 18.7 ya watoto wote wanadaiwa kutumikishwa kwa njia moja au nyingine, hawa wanatumikishwa katika mashamba makubwa, migodini hasa ya wachimbaji wadogo wadogo, majumbani, kwenye shughuli za uvuvi, na hata kwenye shughuli haramu za ukahaba.
Inakadiriwa kuwa kiasi cha watoto milioni 65 kusini mwa jangwa Sahara barani Afrika wanatumikishwa; hii ni asilimia kubwa ya watoto milioni 215 wanaotumikishwa duniani kote. Idadi hii inakaribia theluthi moja ya watoto wote wanaokumbwa na madhila haya duniani.
Kimsingi ajira kwa watoto ni matokeo ya mambo mengi ndani ya jamii, lakini kubwa ya yote ni kuyumba kwa familia kiasi cha kushindwa kulea watoto ipasavyo kiasi cha ama baadhi ya wazazi, ndugu au jamaa kuamua kuwageuza vitegauchumi kwa kuwatuma kutafuta fedha.
Hali hii inachangiwa sana na umasikini katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Kukosekana kwa mifumo dhabiti ya kusimamia na kulinda haki za watoto kumesababisha watoto kutumikishwa kwa kuwa ndiyo njia ambayo inadhaniwa kuwa itasaidia kuwapatia chakula na mahitaji mengine yao au ya familia au walezi wao.
Jamii kwa upanda wake ama imekuwa sehemu ya mfumo huu dhaifu wa kutokulinda haki za watoto kwa yenyewe kuruhusu hali hii kutokea au kuchelea kukemea kwa kuwa imekubalika kuwa utumikishaji wa watoto ni haki.
Ingawa serikali imekuwa ikiibuka na sera, sheria na kauli mbiu na matamko mbalimbali vikilenga kuwalinda watoto, pamoja na kuwako kwa wizara inayojishughulisha na mambo ya watoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, bado usalama wa watoto wengi nchini siyo wa uhakika kwa maana ya kuhakikishwa mahitaji yao yote ndani ya jamii.
Siku hizi ni nadra sana kupita katika miji mikubwa ya nchi hii bila kukutana na watoto wanaodaiwa kuishi katika mazingira magumu, ama wakijishughulisha na kazi ndogo ndogo za kuwapatia ujira wa kujikimu kama kuosha magari, kupaa samaki, kuendesha mikokoteni ya mizigo katika maeneo ya masoko, ilhali wengine wakiomba fedha kwenye makutano ya barabara.
Ni jambo la bahati mbaya zaidi kwamba watoto wengi wamekuwa wanatumikishwa kwenye maeneo ya hatari sana kama vitani na kwenye madanguro yasiyorasmi, kote huko athari siyo za muda mfupi tu bali za maisha kwani mbali ya kuwanyang’anya haki yao ya kuishi kama watoto wakipata matunzo ili wakue katika mkondo unaotakiwa na jamii, huishia kuwa wahalifu sugu na hata kuambukizwa magonjwa hatari kama Ukimwi.
Watoto wanaotumikishwa majumbani nao wamekuwa wanakumbwa na madhila makubwa yasiyoelezeka; wapo wenye nyumba wanaowageuza watoto hawa viburudisho vya tamaa zao za mwili. Lakini pia wapo wanaowatumikisha watoto hawa kwa ujira kiduchu mno na kuwabebesha majukumu makubwa na mazito; kimsingi watoto wanaotumikishwa majumbani wengi wao wanatofauti ndogo sana na watumwa.
Katika miaka ya hivi karibuni tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Ukimwi ambao umesababisha vifo vya watu wengi, hasa wazazi katika familia na kuacha watoto yatima katika umri mdogo, haki za watoto zimekuwa na changamoto kubwa zaidi kuliko zamani; ni kawaida kabisa ndugu kuachiwa watoto yatima wengi wa ndugu zao waliotangulia mbele ya haki, na kwa kuwa umasikini bado ni mkubwa katika jamii yetu, uwezo wa kuhimili mizigo hiyo umekuwa ni mdogo na hivyo kuwasukuma watoto katika ajira mbaya wakiwa wangali wadogo sana.
Tunaamini kuwa taifa linatambua kuwa ajira za watoto ni tatizo kubwa nchini na ni kwa maana hiyo tunafikiri pamoja na kuwapo kwa sheria ya haki za watoto kama hakuna mfumo uliowazi kwa ulinzi wa haki hizi ambao umejengeka kuanzia kwenye ngazi ya taifa hadi kwenye kaya (familia), bado balaa ya ajira kwa watoto itaendelea kuandama taifa hili.
unapoadhimisha siku ya kukataa ajira kwa watoto, tutafakari zaidi jinsi ya kufanya sera na sheria zetu zitekelezeke katika kuwalinda watoto.