


.jpg)
Kocha wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars), Boniface Mkwasa, ambaye timu yake juzi iliiaga michuano ya kimataifa ya Afrika amesema kuwa ili kupata wachezaji wapya wenye uwezo ni lazima kuwepo na ligi ya wanawake nchini.
Twiga Stars ilitolewa na Ethiopia kwa jumla ya magoli 3-1 na hivyo kukosa tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazochezwa mwezi Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Mkwasa alisema kwamba uwezo wa wachezaji wake juzi ulionekana umefikia kikomo tatizo ambalo alishaligundua lakini akakosa wachezaji mbadala wa kuwaita kujaza nafasi hizo.
Mkwasa alisema kwamba wachezaji alionao ni wa muda mrefu na wengine wamekuwa wakishindwa kufanya mazoezi na klabu zao kutokana na matatizo mbalimbali na hufanya mazoezi ya kila siku pale wanapokuwa kwenye kambi ya taifa.
Aliongeza kwamba wapinzani wao Ethiopia walijiandaa vyema kucheza kwa bidii na waliwapa nafasi ya kutawala soka zaidi katika kipindi cha pili ambapo walifanikiwa kupata goli lililowaongezea nguvu ya kufanya mashambulizi.
Nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili, alisema kuwa amesitika kuona wanatolewa kwenye mashindano hayo mwaka huu lakini akaweka wazi kwamba baadhi ya wachezaji walishindwa kujituma kikamilifu kwenye nafasi zao.
Mwasikili alisema kwamba katika kipindi cha pili walielemewa zaidi na walionekana kuchoka na hivyo kuwapa nafasi wapinzani wao watawale mpira.
"Tuliwaruhusu wachezee mpira, na vile vile sisi tulishindwa kujituma zaidi na kucheza kiwango cha chini, kuna wachezaji nilikuwa nawakumbusha waibebe timu lakini sikuona wamebadilika," aliongeza nahodha huyo ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Uturuki.
Twiga Stars ilianza vyema safari ya kuelekea kwenye fainali hizo mapema mwaka huu kwa kuifunga Namibia magoli 7-2 na ilicheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Zimbabwe na Afrika Kusini kabla ya kuivaa Ethiopia.