



Sakata la walimu 500 waliokosa mishahara ya mwezi uliopita kutokana na ajira zao kusitishwa kimakosa, limechukua sura mpya, baada ya Wizara ya Fedha kujivua jukumu hilo na kuitupia lawama Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza na NIPASHE jana, Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, alisema wao walishatoa fedha kwa ajili ya mishahara ya walimu na kwamba wanaopaswa kujua zipo wapi ama zimetumikaje ni Utumishi.
“Sisi tunaletewa mahitaji mengi na hizi fedha za walimu nazo tuliletewa na tuliishalipa sasa kama hawakulipwa sisi hatuhusiki tena na suala hilo” alisema Mduma.
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma jana ilipoulizwa kuhusiana na sakata hilo haikuwa na majibu yoyote.
Utumishi walimwambia Mwandishi kama anataka kujua undani wa sakata hilo aandike maswali na kuyapeleka kwao ili aweze kujibiwa na kwamba bila hivyo haiwezekani kujibiwa bila kufuata utaratibu huo.
Hata hivyo, katika Wizara nyingi na taasisi za serikali wamekuwa wagumu kutoa majibu baada ya kupelekewa maswali kwa njia ya maandishi.
Walimu hao walikumbwa na adha hiyo baada ya majina yao kudaiwa kuwa yalikuwa hewa kufuatia uhakiki wa watumishi wa serikali uliofanywa hivi karibuni.