Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Madaktari wagoma

24th June 2012
Print
Comments
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi

Mgomo ulioitishwa na madaktari nchi nzima kuanzia jana, umeonekana kutekelezwa katika baadhi ya hospitali nchini huku zingine madaktari wakiendelea na kazi kama kawaida.

Hospitali ambako mgomo huo umeonekana dhahiri ni hospitali za mkoa wa Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro na hali imeonekana shwari katika mikoa ya Singida, Dodoma, Arusha, Tanga na Dar es Salaam ukiacha hospitali ya Muhimbili ambako ulionekana mgomo wa chini chini.

Uchunguzi unaonyesha kuwa wale walioendelea na kazi wanadai kuwa hawaoni sababu ya mgomo lakini wanajikuta wakiburuzwa na madaktari wakubwa.

Kwa upande wa Dar es Salaam, mgomo huo umeonekana kuwaathiri wagonjwa wanaopata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini wale wanaotibiwa hospitali za Temeke, Ilala na Mwananyamala, wanaendelea kuhudumiwa na madaktari wao.

Kutokana na hali hiyo, askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), walionekana kuhamisha wagonjwa wao kutoka wodi ya Kibasila katika hospitalini ya Muhimbili na kuondoka nao. Hata hivyo, kitengo cha dharura kilionekana kupokea wagonjwa kama kawaida.

Timu ya waandishi wa NIPASHE Jumapili iliyofika katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam ilikwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili na kushuhudia huduma kudorora na baadhi ya wagonjwa wakilalamika kutoonana na madaktari licha ya kupewa ahadi ya kuonana nao.

“Tulisikia madaktari watagoma, inawezekana tayari wameanza mgomo huo, kwani tangu asubuhi mgonjwa wangu hajatembelewa na daktari yeyote zaidi ya kushughulikiwa na wauguzi,” alisema mmoja wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo.

Hata katika kitengo cha mapokezi, ilishuhudiwa hakuna mhudumu yeyote wa hospitali hiyo wala mgonjwa aliyetakiwa kuhudumiwa, licha ya mmoja wafanyakazi hospitalini hapo kuulizwa, na kusema huduma kwa leo (jana) hakuna.

Wakati mgomo huo ukionekana kuanza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha dharura kilionekana kuendelea na kazi kama kawaida.

“Kitengo cha dharura kimepewa kuendelea kufanya kazi kwa leo tu (jana), lakini kesho (leo), shughuli zote zitasimama,” alisema daktari mmoja aliyeomba kutotajwa jina lake.

Lakini wakati mgomo huo ukionekana kuanza kuvuta kasi Muhimbili, hospitali ya Manispaa Temeke, hali ilikuwa tofauti kwani huduma kwa wagonjwa ziliendelea kama kawaida huku madaktari wote wakiwepo kazini.

Akizungumza na gazeti hili, Ally Ramadhani aliyelazwa wodi ya wanaume hospitali ya Temeke, alisema wanashukuru Mungu kwa kuweza kuhudumiwa na madaktari waliopuuzia mgomo huo.

“Kama unavyoona, hapa hakuna mgomo wowote, na madaktari wanaendelea kutuhudumia kama kawaida, hao waliogoma ni wa huko huko kwingine,” alisema Ramadhani.

“Katika mgomo wa awali, tulidhani tutanufaika, lakini walionufaika ni madaktari wakuu (MD), lakini wale wasaidizi na wauguzi, hakuongezea chochote na serikali…sasa kwanini tugome wakati hatuna manufaa nao,” alisema mmoja wa madaktari hao.

Alisema, ingawa hospitali ya Temeke ina madaktari wakuu (MD) nane, lakini wote hao wameungana na wengine kuendelea kufanya kazi bila kishawishi chochote cha kuunga mgomo ulioitishwa na madaktari.

Aidha, madaktari hao wamesema wameamua kuendelea na kazi kutokana na kuepusha na madhara ambayo yanaweza kuipata jamii, wakiwemo wao ambao nao wana ndugu zao wanahitaji kupata huduma ya afya nchini kote.

Katika Hospitali ya Manispaa ya Ilala, kumekuwa na utofauti wa huduma kwa madaktari kutokana na madaktari (MD) kuitikia wito wa mgomo, huku wasaidizi (AMO) na wauguzi wakiendelea na kazi kama kawaida, hali iliyofanya wagonjwa kuendelea kupewa huduma wanazostahili.

Aidha, hospitali ya Mwananyamala iliungana na hospitali nyingine za jijini la Dar es Salaam, kuendelea kutoa huduma kama ilivyo kwa Temeke na Ilala.

JUMUIYA YA MADAKTARI MSIMAMO PALE PALE

Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema kuwa mgomo wao uko pale pale na kwamba amri iliyotolewa na mahakama haiwahusu na pia hawaitambui.

Alisema amri hiyo wamekuwa wakiisikia katika vyombo vya habari wao haijawafikia na hivyo kufanya wasiitambue.

"Mahakama inasema huu mgomo sio halali sisi haituhusu hiyo order (amri) yao na kwamba tumeshasema mgomo wetu hauna kikomo mpaka serikali iamue kututekelezea madai yetu," alisema Dk Ulimboka.

Alisema madaktari wana matatizo mbalimbali ambayo serikali imeyakimbia badala ya kuyafanyia kazi ili wananchi waweze kupatiwa huduma bora.

Alisema katika Hospitali ya Muhimbili kuna kipimo kwa ajili ya kuchunguza magonjwa mbalimbali (CT Scan) ambacho mpaka sasa ni zaidi ya miezi saba kimeharibika hali ambayo inawasababishia wagonjwa kushindwa kupatiwa huduma hiyo.

Alisisitiza kuwa mgomo wao ni kwa ajili ya kuhakikisha huduma za hospitali zinakuwa katika kiwango kizuri pamoja na madai yao juu ya nyongeza ya mshahara ili wawe wanafanya kazi katika mazingira bora.

RC DAR ES SALAAM ASEMA HAKUNA MGOMO

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik, alisema kufuatia Chama cha Madaktari (MAT) kutangaza kuanza kwa mgomo wa madaktari nchi nzima mkoa huo umefuatilia kwa ukaribu na kubaini kuwa hospitali zote za serikali zimeendelea kutoa huduma kwa wananchi kama kawaida.

Alisema kuwa hakuna taarifa zozote za kugoma kwa madaktari katika hospitali za Mwananyamala, Kinondoni, Temeke na hospitali ya Taifa ya Muhimbili

DK HUSSEIN MWINYI ANENA

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, ameendelea kuwasihi madaktari nchini kuendelea na kazi kama kawaida badala ya kukiuka amri iliyotolewa juzi na Mahakama Kuu ya Tanzania Kitendo cha Kazi.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu, Dk Mwinyi alisema kuwa hadi kufikia jana mchana taarifa walizokuwa nazo ni kwamba, madaktari ambao hawajafika kazini ni wale ambao wapo kwenye mafunzo ya vitendo.

“Baada ya kupata taarifa kuwa leo kutakuwa na mgomo wa madaktari, wizara yangu ilifanya jitihada za kuwasiliana na waganga wasaidizi wa hospitali mbalimbali nchini kujua hali ikoje, taarifa tulizopata shughuli zinaendelea kama kawaida lakini madaktari waliopo kwenye mafunzo ya vitendo ndio hawajafika hospitalini,” alisema.

Alipoulizwa hatua gani zitachukuliwa dhidi ya watu hao, Dk. Mwinyi alisema kufuatia amri iliyotolewa juzi na Mahakama Kuu dhidi ya mgomo huo, wanaiachia mahakama hiyo ichukue hatua zaidi za kisheria.

KCMC WAANZA MGOMO

Madaktari katika hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, wameanza mgomo rasmi ikiwa ni njia ya kuishinikiza serikali kukamilisha madai yao wanayosema ni ya msingi.

NIPASHE Jumapili, ilifika hospitalini humo na kubaini kuwa baadhi ya madaktari wanaendelea na kazi huku wengione walishaweka zana chini tangu ilipofika majira ya saa 6 usiku na kwamba mgomo huo utapamba moto Jumatatu siku ambayo ina wagonjwa wa nje lakini kwa siku za mwisho wa wiki madaktari wengi wapo mapumziko.

Wakizungumza na NIPASHE Jumapili, baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini humo katika wodi ya watoto walisema kuwa, jana walitangaziwa kabisa kuwa kuanzia leo (jana) kutakuwa na mgomo hivyo wagonjwa wenye nafuu waliruhusiwa kutoka hospitalini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka hospitalini humo,

Menejimenti ya hospitali hiyo ilikutana na madaktari bingwa na kuzungumza nao, ili kuwasihi kufanyakazi ambazo zinafanywa na madaktari walio kwenye mgomo ili kuokoa jahazi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka,

akizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu, alisema mgomo upo pale pale na kwamba walishapeleka madai yao ya msingi serikalini

ambayo inapaswa kuyafanyia kazi kikamiluifu na si kama ilivyojibu sasa.

Mmoja wa daktari ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema tangu majira ya saa 6 usiku alishaweka zana chini, na kwamba wachache sana ndio wanaendelea na kazi na wengi wakiwa ni wale ambao imani zao za dini haziwaruhusu kugoma kama watawa, mapadri na wachungaji.

TANGA WAENDELEA NA KAZI

Wakati madaktari wakiendelea na mgomo katika baadhi ya mikoa hapa nchini, hali imekuwa tofauti katika hospitali za mkoa wa Tanga ambapo madaktari wameonekana wakiwepo kwenye vituo vyao vya kazi kama kawaida na kusababisha ugumu wa kubashiri iwapo wapo kwenye mgomo au la.

Katika uchunguzi wa gazeti baadhi ya madaktari wameonekana kutokuwa na maamuzi ya nini cha kufanya kutokana na madai ya kutopokea taarifa yoyote ya mgomo katika vyombo vinavyotambulika kisheria .

“Hatuwezi kusema tumegoma au hatukugoma kwa sababu mpaka sasa hakuna mwelekeo wowote na leo ni week end wengi wapo majumbani lakini mpaka Jumatatu tutakuwa na msimamo wa pamoja kimsingi hizi ni haki zetu na lazima tujitetee,“ alisema mmoja wa madaktari katika moja ya hospitali za mkoani hapa kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Hata hivyo akizungumzia hali hiyo Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) mkoa wa Tanga, Jacob Barnabas, alisema kuwa mpaka sasa hajapokea taarifa zozote za kuwepo kwa mgomo wa madaktri katika hospitali za mkoa huo.

“Nimekuwa nikiwasiliana na wenyeviti wangu wa matawi lakini hakuna hata mmoja aliyenipa taarifa za kuwepo kwa mgomo sasa ngoja tuone mpaka jumatatu hali itakuaje lakini leo wanaendelea na kazi kama kawaida”,alisema Barnabas.

Alisema kuwa ofisi ya Tughe mkoa haijapokea barua yoyote kutoka makao makuu inahusiana kutakiwa kufanya mgomo wa watumishi hao .

MBEYA MADAKTARI WAFUNGA OFISI

Madaktari mkoani Mbeya wamekiuka amri ya Mahakama ya Kazi nchini na kuanza mgomo uliosababisha huduma za afya katika hospitali za Serikali Jijini Mbeya kusuasua.

Katika Hospitali ya Rufaa Mbeya ofisi za madaktari zilikuwa zimefungwa jana asubuhi na kusababisha msongamano wa wagonjwa katika eneo la mapokezi ya hospitali hiyo, ambako wauguzi waliokuwa zamu walikuwa wakiwaandikisha wagonjwa lakini wakishindwa kuwapa maelekezo ya wapi waende kupata huduma.

Nje ya hospitali hiyo na ile ya wazazi iliyopo eneo la Meta mjini hapa, NIPASHE Jumapili lilishuhudia kukiwa kumebandikwa matangazo ambayo yalionyesha kuwa hapatakuwepo na huduma kutokana na kuanza kwa mgomo wa madaktari.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky, alisema kuwa madaktari walioingia kazini jana walikuwa ni 10 tu kati ya madaktari 80 waliopo hospitalini hapo.

Hata hivyo, Dk. Samky alisema kuwa ana uhakika kwamba idadi ya madaktari watakaoendelea na kazi itaongezeka Jumatatu kwa vile jana ilikuwa ni siku ya mapumziko.

Baadhi ya akina mama waliolazwa na watoto wao katika Hospitali ya Rufaa Mbeya wameitaka Serikali kuharakisha kushughulikia tatizo hilo ili kuepusha vifo vinavyoweza kutokea kutokana na wagonjwa kukosa huduma za madaktari waliogoma.

Kwa mujibu wa matangazo yaliyobandikwa kwenye mbao za matangazo na kwenye kuta nje na ndani ya hospitali ya Rufaa Mbeya na ile ya Wazazi Meta, mgomo huo umeanza baada ya majadiliano kati ya serikali na kamati ya madaktari kushindwa kufikia muafaka, hivyo kamati maalum ya madaktari imeamua kutangaza mgomo usiokuwa na kikomo kwa kusitisha utoaji wa huduma kuanzia jana, Juni 23, 2012.

Taarifa hiyo pia iliwataka wananchi wenye matatizo ya kiafya wakatafute huduma sehemu nyingine ili waweze kupata huduma.

Baada ya kutembelea wodi ya watoto nambari 5 na 6 mwandishi wa habari hii alishuhudia wazazi wa watoto wakiwa wamekaa vikundi wakiwa na nyuso za huzuni huku wakionyesha hofu ya watoto wao kupata matibabu kutokana na mgomo huo.

Baadhi ya wauguzi waliokuwa katika mawodi na kuendelea kuhudumia wagonjwa walilazwa hospitali, walikataa kuzungumzia hali ya wagonjwa kukosa huduma za madaktari kwa madai kuwa wao sio wasemaji, ingawa walilalamika kuwa kutokuwepo kwa madaktari kazini kunasababisha na wao washindwe kufanya kazi zao kwa ufasaha.

MWANZA MADAKTARI ZAIDI YA 200 WAGOMA

Madaktari zaidi ya 200 waliopo katika Hosptali ya Rugfaa ya Bugando jijini Mwanza jana wameanza mgomo rasmi baada ya serikali kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu madai yao mbalimbali yaliyosababisha madaktari hao kugoma mapema mwaka huu.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili jijini hapa jana, mwakilishi wa kamati ya kufuatilia madai ya madaktari hao, Dk.Richard Kirita alisema kwamba madaktari wa kada zote katika hospitali hiyo wapo kwenye mgomo isipokuwa baadhi ya madaktari bingwa pamoja na wakuu wa idara.

Hata hivyo, alisema kwamba wanaendelea na vikao ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na wenzao wa Dar es Salaam ili kujua ni hatua zipi zaidi wachukue kuhusiana na mgomo wao huo.

Alisema kwamba katika kikao cha madaktari wa Bugando kilichofanyika hivi karibuni kilihusisha jumla ya madaktari 202 kwa ajili ya kujadili hatma ya madai yao kwa serikali ambapo walikubaliana kwa pamoja kuanza mgomo ifikapo Juni 23 (jana) iwapo madai yao yangekuwa hajatekelezwa na serikali.

Baadhi ya watu waliokuwa wamepeleka wagonjwa katika hospitali hiyo jana walionekana wakiwaondoa baada ya kukosa huduma kutoka kwa madaktari ambao baadhi walikuwa kwenye kikao na wengine walionekana katika vikundi vikundi wakipiga soga.

ARUSHA HALI SHWARI

Hali ya huduma katika hospitali ya Mount Meru katika Mkoa wa Arusha ni shwari, licha ya madaktari kutangaza mgomo nchi nzima.

NIPASHE ilishuhudia wagonjwa wakipata huduma stahili katika hospitali hiyo na zahanati zake za Kaloleni na Levolosi bila kuwepo kwa manung'uniko yoyote toka kwa wagonjwa.

Akizungumza na NIPASHE mmoja wa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa ya Mounti Meru, John Samweli, alisema kuwa alifika katika hospitali hiyo asubuhi jana na amepokelewa vizuri na kupatiwa huduma bila kupata shida.

John aliomba serikali kutfakari kwa makini na kucha kutoa majibu mepesi kwa madaktari hao wanaodai stahiki zao, ambazo walikubalina na serikali na hawajapata.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Eliringia Mlay akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu ya kiganjni, alijibu kwa ufupi kuwa mgomo haupo.

SINGIDA MAMBO SHWARI

Huduma za tiba katika hospitali ya mkoa wa Singida na za Wilaya ya Manyoni, Iramba na Halmashauri ya wilaya ya Singida zimeendelea kama kawaida kinyume na ilivyotangazwa kwamba kutakuwa na mgomo wa madaktari nchi nzima.

NIPASHE ilifika katika hospitali hizo na kushuhudia shuguhuli za huduma za afya zikiendelea kama kawaida huku wauguzi na madaktari wakiwa katika nyuso za furaha wakidai kuwa mgomo huo hauwahusu labda wenzao wa jijini Dar es Salaam na mikoa mingine mikubwa.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi katika hospitali ya Singida, Dk. Joseph Malunda, alisema kimsingi hakuna mgomo wowote na shughuli za tiba zinaendelea kama kawaida.

Mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Fatma Mitigo alisema tangu alipofika hospitalini hapo amepatiwa matibabu kwa wakati.

DODOMA MSWANO

Licha ya madaktari mkoani Dodoma kutoa msimamo wa kuunga mkono mgomo wa kitaifa wa madaktari, huduma za matibabu katika hospitali ya mkoa zimeendelea kama kawaida.

Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili uliohusu mahojiano na baadhi ya wagonjwa mawodini na Mganga Mkuu wa Hospitali Dk. Ezekiel Mpuya, ulibaini kuwa hakukuwa na mgomo jana.

Baadhi ya wagonjwa wa wodi namba 16-A wanaosumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari walieleza kuwa walionwa na matabibu, walipata dawa na wauguzi wa zamu wamekuwa wakiwahudumia.

Katika wodi ya watoto pamoja na ya wazazi hali ilikuwa shwari , shughuli ziliendelea kama kawaida. Kwa upande wake Mganga Mkuu, alisema hakuna aliyegoma na huduma zinaendelea kutolewa .

Ripoti hii imeandaliwa na Beatrice Shayo, Moshi Lusonzo, Romana Mallya, Daniel Mkate, Dar es Salam, Salome Kitomari, Moshi, Lulu George,Tanga, Emmanuel Lengwa, Mbeya, George Ramadhan, Mwanza, Cynthia Mwilolezi, Arusha, Elisante John, Singida na Paulo Mabeja, Dodoma

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment