Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Madaktari 83 Dodoma, Mbeya watimuliwa  

29th June 2012
Print
Comments
Waziri wa Afya Mh. Dkt. Hussein Mwinyi

Uongozi wa Hospitali ya Hospital ya Mkoa wa Dodoma pamoja na wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, umewasimamisha madaktari waliokuwa kwenye mgomo na kuwataka waripoti kwa Katibu Mkuu (Utumishi).

Mkoani Dodoma, uongozi huo umewasimamisha kazi madaktari 11 wa mafunzo kwa vitendo kutokana na kuendelea na mgomo.  

Akizungumza na NIPASHE jana Mwenyekiti wa Kamati ya Jumuiya ya Madaktari Mkoa wa Dodoma Dk. Cassian Mkuwa, alithibitisha kufukuzwa kwa madaktari hao akiwemo yeye.  

Mkuwa alisema tukio la kufukuzwa kwa madaktari hao limetokea jana asubuhi wakati wakiwa hospitalini hapo wakiendelea na mgomo wao.  
 
Alisema mara baada ya kufika Hospitalini hapo Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Ezeliel Mpuya, aliwaita madaktari wote waliopo katika mafunzo kwa nia ya kuzungumza nao na kutoa barua kwa madaktari 11 na kudai kuwa hao wamesimamishwa kazi kuanzia jana kutokana na mgomo.  

Alisema Madaktari waliosimamishwa kazi walikataa kupokea barua hizo na kutakiwa kuondoka katika eneo la Hopsitali hiyo.
 
“Nashindwa kuelewa ni vigezo gani vilitumika kuwapata madaktari hao 11 na kuwasimamisha kazi kwani walikuwa wakigoma ni zaidi ya madaktari 20,” alisema.  
 
Dk. Mkuwa alisema wameshatuma taarifa kwa Kamati Kuu ya Jumuiya hiyo jijini Dar es salaam kwa ajili ya hatua zaidi.  
 
Akizungumzia suala hilo, Mpuya alisema hajui tukio lolote kwa sasa na kudai kuwa anachojua ni kuwa wao wamegoma hivyo hawana sababu ya kuwepo hospitali.  

Mkoani Mbeya, taarifa zinaeleza kwamba madaktari 54 walio kwenye mafunzo kwa vitendo pamoja na 18 waliosajiliwa wamesimamishwa kazi kwa kudaiwa kushiriki mgomo.

Ilielezwa kwamba wametakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi ili aweze kuwapangia vituo vingine vya kazi.

Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, Mbeya na Paul Mabeja, Dodoma.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment