Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Serikali ijitahidi kupambana na mgomo wa madaktari

1st July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea katika hospitali mbalimbali nchini, Serikali imejizatiti kuimarisha huduma ya tiba kwa kutumia hospitali za Jeshi, binafsi pamoja na kuwaita madaktari wastaafu ili kunusuru afya za wagonjwa.

Awali hospitali zilizokubali kushirikiana na Serikali katika kuokoa maisha ya Watanzania watakaohitaji tiba ya haraka na wale walio katika tiba isiyoweza kusitishwa ni pamoja na TMJ, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT na hospitali ya Jeshi ya Lugalo. Serikali pia imeongeza nguvu katika hospitali za Mwananyamala, Amana , Temeke zote za jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja mwishoni mwa wiki alisema hatua zote hizo zimetokana na utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu ambapo agizo hilo limeanza kutekelezwa na sasa nguvu imeelekezwa hadi kuhusisha hospitali binafsi, na kwamba wanaendelea kuongea na hospitali zingine.

Mwamwaja pia alifafanua namna ya wagonjwa watakavyopata huduma za tiba katika hospitali hizo za binafsi, kwamba kutakuwa na fomu maalum ambayo madaktari wa Amana, Mwananyamala au Temeke watakapoona mgonjwa anahitaji tiba kubwa zaidi, watamjazia ili aweze kupokelewa katika hospitali hizo.

Pia kwa wagonjwa ambao watahitaji rufaa, kwa utaratibu huo huo watatibiwa katika hospitali ya Jeshi iliyoko Lugalo ambayo alisema imekuwa tayari muda mrefu ikishirikiana na hospitali nyingine zilizoko chini yake.

Katika mgomo wa madaktari uliofanyika mara ya kwanza, Mwamwaja anasema madaktari waliopelekwa Muhimbili kutoa huduma baadhi yao walikwamishwa kwa makusudi na madaktari wenyeji ili wasitoe huduma ipasavyo, kutokana na hali hiyo serikali ililiona hilo na ndio maana imeamua wagonjwa wapelekwe huko huko kwenye hospitali za jeshi na binafsi ili kupata tiba vizuri zaidi.

Sisi tunaona hatua hizi ni njema na kwa dhati tunazipongeza kwa serikali kuona ulazima wa kuingia gharama za kuweka mkataba na hospitali binafsi ili kuokoa maisha ya Watanzania ambao wangeweza kupoteza maisha kwa kukosa tiba stahiki. Ni vema pia serikali ikaanzisha utaratibu kama huo kwa maeneo mengine huko mikoani ambako kuna migomo ya madaktari kama hiyo.

Hali kama hii ni ya dharura, taifa linapoingia katika hali ya dharura suala la gharama halipaswi kuhojiwa hasa linapokuja suala la kuokoa uhai wa watu wanaojikuta katika adhabu wasiyostahili.

Mgomo wa madaktari ni suala linaloweza kutatuliwa kwa hatua mbalimbali, linaweza kusubiri muafaka, lakini maisha ya mgonjwa hayana mjadala wa kusubiri, na hilo ndilo serikali ililoliona kwanza wakati majadiliano na madaktari kuhusu madai yao yakiendelea.

Athari za mgomo wa madaktari ni kubwa, ikiwa ni pamoja na vifo, na siyo rahisi kupima athari zake kwa kuthaminisha na kitu chochote, maisha ya binadamu yanapotoweka siyo rahisi kuwepo na mbadala, na hayalinganishwi kwa thamani na kitu chochote, na ndio maana Serikali inachukua kila hatua muhimu ili kuyanusuru maisha ya wananchi wake.

Tunaipongeza serikali kwa hatua zote inazozichukua, na pia tunawasihi madaktari wasitishe mgomo huo kwani kimsingi serikali iliahidi kuyatekeleza madai yao yote kwa kutegemea uwezo wa kibajeti na hali ya uchumi iliyopo.

Madai ya madaktari yanaweza kutekelezwa, ila wakati huo huo madaktari nao kama binadamu na Watanzania wenye uchungu na uhai wa binadamu wenzao, warudi kazini wakati Serikali ikiendelea kuweka sawa masuala ya madai hayo. Ikumbukwe huu ni wakati wa Bajeti na Wizara ya Afya itakapoleta bajeti yake Bungeni suala la madai yao linaweza kuwa tayari sehemu kubwa limepatiwa ufumbuzi. Siku zote subira yavuta heri.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment