


Ulimi ni kiungo kidogo katika mwili wa mwanadamu lakini ukitumika vibaya unaweza kubashiri mema ama kuacha laana.Yote yawezekana ingawa kwa muungwana ana desturi ya kuomba mema siku zote.
Muungwana huyo ulimi wake hunena taratibu lakini huwa na macho angavu zaidi ya sayari ya jua. Ndiyo! binadamu ameumbwa akapewa utashi wa kutambua siku moja atakumbwa na mauti ingawa hakupewa uwezo wa kufahamu ni lini kifo hicho kitamkuta.
Anaondoka akijua na kufahamu kwamba taifa lake linaweza kukua kiuchumi au kuanguka kiuchumi siku moja lakini mawazo yake yakaendelea kuishi.Mawazo yanaishi na kuwa na thamani zaidi ya kifo.
Kwa mantiki hiyo,yatupasa kuwa wa kweli na wazalendo kwa taifa letu, yamkini itamgarimu au laa. Kama ndivyo, sina budi kuyazungumza yale yanayoipa nafasi ya furaha au simanzi moyo wangu kuhusiana na uvunaji wa rasilimali za taifa.
Hivi sasa serikali imo katika furuha kubwa baada ya kamati ya urithi wa dunia iliyopo chini ya Shirika la Elimu,Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Uniseco) kuridhia kumegwa kwa pori la akiba la Selous.
Kwa katiba ya nchi yetu, Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo yenye dhamana ya kusimamia rasilimali za taifa hili zikiwemo hifadhi,migodi ya dhahabu,madini, amali mbalimbali za asili na hata zile za kutengenezwa na wanadamu kwa uweza wa muumba wao.
Natambua kwamba fursa ndogo ni mwanzo mzuri wa mafanikio makubwa kwa kuwa ni wazi kwamba, kibali kilichotolewa na Unesco kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya uranium katika pori la akiba la Selous kitalinufaisha taifa na kulifanya likue kiuchumi kutokana na mapato yatokanayo na uchimbaji huo. Katika hilo sina matatizo nalo isipokuwa mwendawazimu peke yake ndiye atakayebisha!
Serikali imetuambia kwamba katika pori hilo eneo litakalomegwa Kusini mwa Tanzania kutokana na kubainika kuwa na kiasi kikubwa cha madini hayo ni km za mraba 200 katika ya km za mraba 50,000 zilizopo Selous.
Na katika harakati hizo la taifa kuvuna rasilimali zake,tayari eneo hilo limekwishayavutia makampuni ya uchimbaji uranium ambapo mojawapo imetenga dola za kimarekani milioni 400 sawa na sh. bilioni 640.
Katika uvunaji huo serikali itaambulia mapato ya sh. bilioni 8 kwa mwaka na wachimbaji wa mradi huo watachuma kiasi cha sh. bilioni 320.
Sawa! serikali itaongeza mapato yake lakini, je? uhamishaji wa rasilimali hiyo kwenda nje ya nchi kuendeleza wengine na kuiacha Tanzania ikisononeka kwa ukiwa,siyo jambo linalowafurahisha wengi wetu!
Nasema hivyo kwa sababu kuu moja kwamba hatukatai maendeleo lakini basi pawepo na umakini katika ufungaji mikataba ya madini kwa kuwa mikataba mingi inayoingia serikali na wawekezaji inalitia taifa hasara kubwa.
Yamkini,wengi ni mashahidi kwa jinsi kumekuwapo na mvutano kuhusu rasilimali za taifa hususani uchimbaji wa dhahabu,tanzanite na hata gesi asili.
Watanzania wenzetu wanafikiri na wanalalama kila wakati kwamba hawanufaiki na matunda ya uvunaji wa rasilimali za taifa kwa sababu ya mitakaba mibovu ambayo inawanufaisha wajanja wachache na hivyo kutengeneza matabaka ya kiuchumi.
Wanahofia matabaka yaliyopo kati ya walionacho, wasio nacho na walalahoi kwamba yataendelea kuwatafuna kutokana na udhaifu huo katika mgawanyo wa rasiliamali za taifa.
Ndiyo maana nauliza swali hili la uchokozi kwamba kama hakutakuwa na umakini katika ufungaji wa mikataba ya madini katika eneo hilo la Kusini mwa Tanzania. Je, uvunaji uranium Selous, hautaivua nguo serikali?
Godfrey Mushi ni Mwandishi wa Habari, Mwakilishi wa NIPASHE mkoani Iringa,anapatikana kwa simu namba 0767 535490 au barua pepe, ghandsome79@hotmail.com