Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nsajigwa nje, Yondani ndani Yanga Kagame

13th July 2012
Print
Comments
Kelvin Yondani

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet jana alimtaja beki wa kati Kelvin Yondani kuwa miongoni mwa wachezaji 20 atakaowatumia katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza nchini kesho licha ya klabu yake ya zamani ya Simba kusema ni mchezaji wake halali.

Hata hivyo, Saintfiet amemuacha nje ya kikosi nahodha Shadrack Nsajigwa aliyekuwa shujaa wakati Yanga ikitwaa kutwaa ubingwa huo msimu uliopita, pamoja na Nurdin Bakari ambaye ni majeruhi.

Akizungumza jana kwenye makao makuu ya Klabu ya Yanga, Saintfiet alisema kuwa ameamua kumuacha Nsajigwa kwa kuwa ana mabeki wengine wawili, Juma Abdul na Godfrey Taita, walioonyesha kiwango kizuri zaidi kwenye mechi mbili za kirafiki za timu hiyo hivi karibuni.

Saintfiet alisema kwamba licha ya kumuacha kwenye mashindano hayo, bado anamuhitaji Nsajigwa kwenye mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara kutokana na uzoefu wake ambao utawasaidia wachezaji chipukizi kujifunza kutoka kwake.

Kocha huyo alisema pia amewaacha wachezaji wengine watatu, Simon Msuva, Omega Seme na Frank Domayo, kutokana na kuwa na jukumu la taifa ambalo linawasubiri kwenye timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) inayokabiliwa na mechi mbili za kirafiki dhidi ya Rwanda (Jumamosi na Jumatatu) na mechi ya vijana ya Afrika dhidi ya Nigeria itakayochezwa Julai 29 hapa nchini.

Saintfiet alisema kwamba kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Kagame na anaamini ushindi katika mechi ya kwanza ya ufunguzi dhidi ya Atletico kutoka Burundi utawaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

"Ni mashindano magumu lakini tuko tayari kupambana, kimwili na kiakili, ila nilikuwa na wakati mgumu katika kuteua viungo, kiukweli tuna viungo bora, ila nimelazimika kuangalia pia na nafasi nyingine ambazo ni muhimu kwenye timu," alitamba kocha huyo ambaye ameiongoza Yanga kwa siku nane.

Alikitaja kikosi chake kamili atakachokichezesha katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na Yaw Berko, Ally Mustapha 'Barthez', David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Yondani, Abdul, Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua, Stephano Mwasika, Athumani Iddi 'Chuji', Rashid Gumbo, Juma Seif 'Kijiko', Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Idrissa Senga, Khamisi Kiiza, Saidi Bahanuzi, Jerry Tegete na Shamte Ally.

Yanga bado ina nafasi mbili za kusajili wachezaji wa kigeni. Klabu hiyo pia imemuacha mchezaji mwingine, Salum Telela, ambaye alivunjika mguu katika mechi za mwisho za msimu wa Ligi Kuu ya Bara.

Wakati huo huo, uongozi wa Simba leo unatarajiwa kutangaza kikosi chake huku habari za ndani zikisema kwamba huenda Yondani pia akatajwa kwenye timu hiyo kutokana na madai kwamba ana mkataba na timu hiyo ambao ulisainiwa Desemba 23 mwaka jana.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment