


.jpg)
Waziri wa Utalii na Maliasili, Balozi Khamis Kagasheki, anatarajiwa kuzindua mradi wa miaka mitano wa hifadhi, utawala na uendelezaji misitu maarufu kama ‘kampeni ya mama misitu’.
Meneja wa kampeni hiyo, Gwamaka Mwakyanjala, alisema utekelezaji wa mradi huo unafuatia matokeo ya mradi wa majaribio uliofanyika kati ya mwaka 2008 na 2010.
Mradi huo unazinduliwa leo, utafanyika katika maeneo ya mikoa iliyopo pwani ya Bahari ya Hindi, miongoni mwao ikiwa ni Kisarawe, Rufiji, Kibaha, Kilwa na Lindi.
Katika uzinduzi huo, wataalam wa masuala ya misitu na watekelezaji wa miradi inayohusu eneo hilo, pamoja na mambo mengine, watajadili na kuelezea uzoefu walionao katika sekta hiyo na namna bora ya kuiendeleza sekta hiyo.
Mwakyanjala alisema mradi huo unaotekelezwa kwa udhamini wa serikali za Norway na Finland, utahusisha wadau mbalimbali kikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).
Aliwataja baadhi ya wadau wengine kuwa ni WWF tawi la Tanzania, Asasi ya Hifadhi ya Mpingo na Asasi ya Hifadhi ya Misitu TFCG.