Saturday Feb 13, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TFDA kuchunguza ARV `feki` ni kesi ya nyani kumpelekea nyani!

30th September 2012
Print
Comments

Karibu wiki yote hii, vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti habari za kusikitisha na kuhuzunisha zinazohusu sakata la kusambazwa kwa Dawa ‘feki’ za Kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV).

Inaelezwa kuwa kiwango kikubwa cha dawa hizo, ambazo hutolewa bure na serikali katika hospitali zake zimesambazwa na maelfu ya wagonjwa wameshazitumia kwa kiasi kikubwa.

ARV hizo ‘feki’ zinazodaiwa kutoka nchini India, ziliingizwa kwenye mfumo tangu Mei, mwaka huu. Ina maana kwamba, hadi kipindi hiki zinaondolewa kwenye mfumo, ni miezi minne imekwishapita tangu zianze kutumiwa na wagonjwa!

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Seleman Rashid, alikaririwa na vyombo vya habari akisema serikali ndiyo iliyogundua kuingizwa kwa ARV hizo ‘feki’ nchini.

Lakini taarifa nyingine zimemkariri mmiliki wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPIL) kinachotengeneza ARV, Zarina Madabida, akisema kiwanda chake ndicho kilichogundua kuwapo kwa dawa hizo.

Zarina, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anasema baada ya kugundua ARV hizo ‘feki’, alitoa taarifa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na kuiomba iingilie kati ili kuziondoa kwenye mzunguko.

Kwa uchache, habari za kuwapo kwa ARV bandia kwenye mzunguko, ni msiba mkubwa kwa ndugu zetu waathirika wa VVU. Kwani sasa wana hofu kubwa kuhusu afya zao.

Hadi taarifa za kusambazwa kwa ARV hizo ‘feki’ zinatangazwa na vyombo vya habari, mpaka sasa bado haijajulikana nini malengo ya wahusika kuingiza dawa hizo ‘feki’ nchini.

Pili, TFDA ndiyo hushughulikia uhakiki wa usalama wa dawa na chakula. Kwamba, kabla dawa au chakula hakijaingizwa ndani ya nchi, ni lazima TFDA iidhinishe ubora wake kwa maisha ya binadamu. Je, ilikuwa wapi wakati ARV hizo ‘feki’ zinaingia nchini.

Tatu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ndiyo msimamizi mkuu wa afya za Watanzania. Haijulikani ina taarifa ni kwa kiasi gani Watanzania wameathirika kwa matumizi ya ARV hizo ‘feki”.

Nne, haijulikani kama TFDA iko tayari kutoa taarifa ya wahusika wote na hatua zilizokwishachukuliwa hadi sasa dhidi ya watu hao.

Tano, ni hasara kiasi gani, ambayo serikali imeipata kutokana na ‘ujangili’ huu. Kwa maana ya fedha zilizoibwa kwa kuingiza dawa hizo ‘feki’.

akati tukitafakari mambo hayo, Naibu Waziri wa Afya, Seif mbali ya kuthibitisha kwamba, ni serikali pekee ndiyo huagiza dawa nje ya nchi, amewataka wananchi kuipa TFDA muda kuchunguza ARV hizo ‘feki’!

Kwa kauli hiyo, naibu waziri huyo ana maana kwamba, hivi sasa TFDA iko katika uchunguzi juu ya ARV hizo ‘feki’.

Wakati TFDA ikichunguza ARV hizo, tayari Dk. Seif amekaririwa akithibitisha kuwa dawa hizo ni ‘feki’. Ikiwa ukweli umekwishajulikana, ni kitu tena kinachochunguzwa na TFDA?

Haidhaniwi kama serikali, hasa wizara, TFDA na vyombo vya usalama vinalazimika kufanya uchunguzi.

Maana katika hali ya kawaida, hakuna kitu cha kuchunguza hapo zaidi ya kuwawajibisha wahusika wote.

Kwani hao ni walafi wachache wanaojali fedha kuliko maisha ya watu. Ni wauaji wa makusudi, wahalifu na pia ni wasaliti wakubwa.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Regina Kikuli, alikaririwa akithibitisha kukamatwa kwa makopo 8,000 ya ARV ‘feki’. Ikiwa ukweli ni huo, ni dhahiri kuwa wahusika wanajulikana.

Kwa jumla, kuna udhaifu mkubwa kwa mamlaka husika katika kudhibiti hujuma kama hiyo.

Rushwa, ufisadi na tamaa za baadhi ya watu kutaka kutajirika ghafla. Yote hayo ndiyo yanayochangia tatizo hilo, ambalo ni mwendelezo kwa Tanzania kuwa jalala la bidhaa mbovu zisizokidhi viwango.

Bidhaa hizo ni kuanzia dawa za binadamu na mifugo, vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, samani za ndani, vyakula, vifaa vya elektroniki, magari mabovu nakadhalika.

Haidhaniwi kuwa bidhaa zote hizo huingizwa na kusambazwa nchini kimazingaombwe au kimiujiza. Pia haidhaniwi kuwa huingizwa kwa kushuka kutoka juu.

Bali hupokelewa kutoka taasisi moja kwenda nyingine kwa utaratibu maalum na unaoeleweka.

Kama nilivyotangulia kueleza hapo juu kwamba, kuna udhaifu mkubwa kwa mamlaka husika.

Matokeo yake ndiyo hayo. Madhara yanampata mwananchi wa kawaida. Hivi sasa mwananchi huyo maskini hana uhakika na afya yake baada ya kulishwa sumu kwa dawa feki!

Kwa hakika, hili ni janga la kitaifa. Leo imetokea kwenye dawa ‘feki’, yawezekana kesho ukawa mchele na keshokutwa unga, au dagaa, au maji nakadhalika. Janga la kitaifa!!!

Kwa hali hiyo, ningependa kusisitiza hatua za kuwajibisha wahusika, ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za uhalifu dhidi ni wakati sasa wa kuchukuliwa.

Pia ningependa niungane na Mkuu wa Idara ya Dawa katika Kitengo cha Ukimwi Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, Charles Lyimo, kwamba, hakuna sababu ya kumtafuta mchawi kwenye tatizo hilo.

Bali serikali ijichunguze yenyewe kwa kuwa dawa hizo ‘feki’ kama alivyosema Dk. Seif hazisambazwi na watu binafsi. Zinasambazwa na serikali.

Serikali hupeleka ‘oda’ kiwandani. Dawa zikishatengenezwa huzikagua kama ziko salama au la. Kisha ndiyo huzigawa na kuzisambaza kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

ARV inaelezwa kuwa zinatengenezwa pia mkoani Arusha kwenye kiwanda kilichopewa kibali na serikali. Kwa maana hiyo, serikali inapaswa kujihoji.

Watanzania kufikia kutumia dawa ‘feki’, ni vigumu TFDA kuepuka lawama. TFDA ni mmoja wa watuhumiwa wakubwa.

Hivyo, hakuna uhalali wa kuipa TFDA kazi ya kuchunguza kadhia hiyo na hasa kinachochunguzwa hakijulikani na imekwishathibitika kuwa kilichoingizwa nchini ni ARV ‘feki’.

Maana kufanya hivyo haiwi tena kesi ya nyani kumpelekea ngedere. Bali inakuwa kesi ya nyani kumpelekea nyani ahukumu!

Hiyo ni sawa na ile kesi, ambayo washtakiwa walikuwa askari polisi waliotuhumiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara wa madini na dereva teksi.

Kiroja kikawa hivi. Kesi inawahusu polisi, mkamataji akawa polisi, mpelelezi polisi, mwenye vielelezo polisi, muandaaji wa mashtaka polisi, aliyewapeleka watuhumiwa mahakamani polisi. Je, hapo kuna japo chembe ya matumaini ya ukweli kujulikana?

Hilo ni swali linalohitaji kukaliwa kitako!

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment