Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Vurugu za Waislamu Dar, Zanzibar: Chadema yaibomoa serikali

21st October 2012
Print
Comments

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeituhumu Serikali kuwa ndiyo inayochochea udini kwenye siasa zinazosababisha vurugu na chuki zilizoenea nchini.

Kadhalika kimeilaumu kuwa imeshindwa kushughulikia madai na malalamiko ya Waislamu kwa miongo mingi hatua iliyochochea vurugu za Waislam  katika miji ya  Zanzibar na Dar es Salaam wiki hii.

Wanasheria waandamizi wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando, walitoa madai hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wanahabari ulioitishwa kuzungumzia vurumai na maandamano ya kidini.

Kuchochea dini kwenye siasa:
Marando alisema serikali ilizua kuwa chama cha CUF ni cha kidini na ni cha  Waislamu  pia inaeneza propaganda kuwa Chadema ni cha Wakristo hasa Wakatoliki.

Aliongeza kuwa madai hayo yanatolewa baada ya CUF kupata nguvu iliyoifanya kuwa tishio kwa CCM na serikali yake  wakati Chadema  inadaiwa kuwa ya kidini baada ya kuibuka kuwa chama tarajiwa chenye mwelekeo wa kutwaa  dola.

Wakizungumza kwa kupokezana, Safari na Marando waliitaka serikali kusikiliza malalamiko ya Waislam  iliyoyapuuza kwa miongo mingi badala ya kulikumbatia Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na kuupuuza asasi nyingine.

Waliitaka kuwakutanisha Waislamu na asasi zote kusikiliza malalamiko yao na kupata ufumbuzi badala ya kutumia jeshi na polisi kuzima maandamano ambayo yanafanyika kutokana na mlundikano wa chuki nyingi zinazotokana na Waislamu kutosikilizwa .

Profesa Safari alisema yapo malalamiko ya Waislam ambayo hajasikilizwa tangu Uhuru na kila siku yanaongezeka mfano wanataka Mahakama ya Kadhi, kujiunga na Muungano wa Nchi za Kiislam (OIC) na pia kushinikiza kipengele cha kutaja imani ya mtu kuingizwa kwenye sensa ya watu na makazi.

Wakizungumzia kutoweka na kuibuka kwa kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar,  Sheikh Farid Hadi Ahmed, waliishangaa serikali ‘kumteka’ na kutangaza kuwa taasisi  za ulinzi na usalama hazijui aliko.

Marando alihoji: “Inakuwaje serikali ijidanganye kuwa haijui alipo Sheikh Faridi na kusababisha  vurugu, kuchoma na kuharibu mali na hata  kifo cha polisi  Said Abdularahman aliyepigwa mapanga kuhusiana na tukio hilo?”

Chadema iliitaka serikali kuwa na uwazi na kueleza alikokuwa Sheikh Farid ambaye aliibuka juzi na kuvieleza vyombo vya habari kuwa alikuwa anahojiwa na Usalama wa Taifa wakati polisi Zanzibar ilisema haijui aliko.

 

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment