Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mwanamke achinjwa kama kuku

23rd December 2012
Print
  *Wauaji waondoka na kichwa chake

Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Kwikuba wilayani Butiama ameauwa kwa kuchinjwa kama kuku na watu wasiojulikana na baadaye kukimbia na kichwa chake.

Watu hao wanadaiwa kabla ya kumuua mwanamke huyo walimkatakata kwa mapanga na baadae kumchinja tukio linaloelezwa kuwa ni mfululizo wa mauaji yaliyoibuka siku za karibuni mkoani humo.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana (Desemba 22), katika kijiji hicho kata ya Mugango ambapo kabla ya wauji hao kufanya unyama huo waliomba kupatiwa simu na fedha kutoka kwa mwanamke huyo.

Imedaiwa kuwa baada ya kukosa vitu hivyo waliomba kupatiwa kichwa cha binadamu na kuanza kumshambulia kwa mapanga mwanamke huyo aliyejulikana kama Tabu Makanya (68) na kumchinja.

Mtoto wa marehemu aliyekuwa amelala na mama yake kitanda kimoja, Nyasinde Marubira (24), aliiambia NIPASHE Jumapili kuwa watu hao wanaosadikiwa kuwa zaidi ya wanne walivunja mlango na kuingia katika nyumba yao na kuwaamuru watoe pesa na simu na baada kuwaambia  hawana vitu hivyo ndipo walipomshambulia mama yake huku yeye akiamuliwa kujifunika kichwa.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya kutokea matukio kadhaa ya watu kukatwa mapanga, kuchinjwa na wauji kuondoka na viungo vikiwemo vichwa.

Alisema watu hao walisikika wakisema “leta panga kata na kisha kata kichwa,” huku mama yake akipiga kelele na baada ya hapo hakusikia tena kelele za mama yake.

Mtoto huyo  akijieleza huku akibubujikwa na machozi alisema baada ya kutosikia sauti ya mama yake na watu waliowavamia kuondoka, aliamka na kumfunua mama yake aliyefunikwa na kumkuta akiwa hana kichwa huku wauji hao wakiwa wameondoka nacho.

“Baada ya hapo niliamua kupiga yowe na wanakijiji kuamka na kuanza kufutilia tukio ndipo walipokuta kichwa hicho kikiwa kimetupwa porini. Kwa kweli nimeumizwa sana na tukio hili la kinyama alilofanyiwa mama yangu mzazi,” alisema mtoto huyo huku akilia kwa uchungu.

Alisema Jeshi la Polisi pamoja na Serikali linapaswa kufatilia kwa kina matukio ya namna hiyo ambapo watu wamekuwa wakiuawa kinyama na kisha kuondoka na viungo vyao huku hakuna hatua zinazochukuliwa.

Tukio hilo lilisababisha wananchi wakiongozwa na wandesha pikipiki maarufu kama bodaboda kuandamana hadi ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara wakimtaka aeleze ni hatua gani zinafanywa na jeshi hilo kukomesha matukio hayo la sivyo ajiuzuru nafasi hiyo.

Hata hivyo maandamano hayo yalikumbana na ulinzi mkazi wa askari wa  kikosi cha FFU waliokuwa na silaha za moto, mabomu ya machozi na  kuwazuia kuingia katika jengo la kamanda huyo.

“Hatutaki, tumechoka, hatutaki, tumechoka, Kikwete uko wapi, Mwema uko wapi” hayo ni baadhi ya maneno yalikuwa yakitamkwa na wananchi hao nje ya lango la ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mara.

Hata hivyo, mkuu wa kituo kikuu cha polisi mjini Musoma aliyejulikana kwa jina la Huppa alifanikiwa kuwaondoa wananchi hao katika eneo hilo baada ya kuwaambia kuwa kamanda wa polisi yuko eneo la hospitali akiwangoja ili wazungumze nao, jambo lilowafanya kuelekea huko na kuwapa nafasi polisi kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Bodaboda hao waliungana na wananchi hao ikiwa ni siku mbili baada ya mwenzao kuchinjwa kwa kutumia shoka tukio lilotokea maeneo ya Kata ya Nyankanga na kumpora pikipiki yake.

“Tumechoshwa na matukio ya mauaji katika mkoa wa Mara wakati vyombo vya usalama vipo tunataka litolewe tamko ni namna gani matukio haya yanashughulikiwa na vyombo vinavyohusika,” alisikika John Magafu mmoja wa madereva hao.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma, alisema kuwa watu wanne wanaojulikana (majina yanahifadhiwa) wanatafutwa na jeshi hilo baada ya kufanya tukio hilo na kukimbia.

Taarifa ya Kamanda Mwakyoma kwa waandishi wa habari ilisema watu sita wanashikiliwa mpaka sasa kufuatia mauji ya aina hiyo likiwemo tukio la mauaji ya Sabina Mkirerikatika aliuawa na kichwa chake kuchukuliwa.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Mara, John Tupa, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, alisema ameiagiza kamati hiyo wilayani Butiama kuchukua hatua ya kukabiliana na mauji hayo ikiwa ni pamoja na kutolala hadi wauaji hao wapatikane.

Alisema kamati hiyo ilikutana jana kupanga mikakati ya kupambana na mauaji hayo na kesho itakutana na viongozi mbalimbali wilaya ya Butiama  kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo alisisitiza viongozi wa vijiji kuimarisha ulinzi wa jamii kwa maelezo kuwa inashangaza kuona kuwa matukio hayo yanatokea ndani ya vijiji huku viongozi wa vijiji na wananchi wakishindwa kujua wauaji.

 
      

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

Articles

No articles