Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nchimbi: Bidhaa za duka lenye msamaha wa kodi zisifanyiwe biashara

10th February 2013
Print

 Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, ameapa kutowavumilia askari magereza ambao wanageuza duka la kuuza bidhaa zenye msamaha wa kodi kuwa sehemu ya biashara ya kujiongezea kipato.

Nchimbi alitoa kauli hiyo juzi wakati akifungua duka hilo lililopo Ukonga magereza jijini Dar es Salaam.

Alisema lengo la serikali kuzindua duka hilo ni kupunguza ughali wa maisha kwa maofisa wa Magereza ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi na sio kuwa sehemu ya biashara kwao.

“Msigeuze duka hili kama sehemu ya mtaji kwa kuchukua vitu na kwenda kuuza mtaani au kufungua biashara, atakayethibitika kafanya hivyo atachukuliwa hatua,” alisema.

Alisema kikao cha Bunge la bajeti cha mwaka 2009/2010 kilipitisha uamuzi wa kupanua wigo wa msamaha wa maduka yasiyotoza kodi ili kujumuisha vyombo vya ulinzi na usalama likiwamo Magereza.

Nchimbi alisema lengo la Serikali ni kuvipa nafasi Vyombo hivyo kuitumikia nchi yao vyema na kwa uaminifu na kujipatia bidhaa kama sementi, mabati, samani na bidhaa nyingine kwa bei nafuu.

Alisema maduka kama hayo ni mpango endelevu wa serikali nchi nzima kuhakikisha kuwa kila eneo yanakuwepo.

Kamishna Jenerali wa Magereza John Minja aliwahimiza askari hao kuwa waaminifu na kusisitiza kuwa maduka hayo yatafunguliwa nchi nzima.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

Articles

No articles