Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tukio la kushambuliwa kwa Kibanda lichunguzwe haraka

7th March 2013
Print
Maoni ya Katuni.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, amefanyiwa unyama wa kutisha baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana waliomteka, kumpa kipigo na kumejuhi vibaya  sehemu kadhaa za mwili wake na kisha kumng’oa meno na kumtoboa jicho.

Tukio hilo ambalo limewashtua wanahabari na wadau wa habari limetokea usiku wa kuamkia jana kati ya saa 6:00 na 7:00 usiku nyumbani kwake eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Unyama aliofanyiwa Kibanda, unafanana na ule aliowahi kufanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, ambaye alitekwa usiku wa Julai 26, mwaka jana na watu wasiojulikana kisha wakamtesa, kumnyofoa kucha na kumng’oa meno.

Akizungumza kwa shida na NIPASHE katika chumba cha dharura cha Taasisi ya Mifupa (MOI), alikopelekwa baada ya tukio hilo, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, alisema alivamiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake ambao kabla ya kumjeruhi, walivunja kioo cha gari lake.

Alisema baada ya kuvamiwa na watu hao na kuanza kuvunja kioo cha gari, alilazimika kurukia kiti cha nyuma cha gari lake lakini watu hao, walimfuata na kumtoa ndani ya gari hilo.

Alisema baada ya kumtoa ndani ya gari, watu hao walimchukua na kumpeleka kusikojulikana mbali na nyumbani kwake na kuanza kumshambulia mfululizo hadi akapoteza fahamu.

Tunaungana na wadau wote wa habari na jamii kwa ujumla kulaani vikali kitendo hiki cha kinyama alichofanyiwa Kibanda.

Kitendo hiki kinapaswa si kulaaniwa tu, bali pia vyombo vinavyohusika na jamii kwa ujumla, kujiuliza nini kinachoendelea nchini mwetu kuhusiana na waandishi wa habari na kuchukua hatua.

Vitendo vya kudhuru au kuua waandishi wa habari siku hizi vinaonekana kuwa jambo la kawaida hapa nchini.

Ikumbukwe kwamba hii si mara ya kwanza kwa waandishi wa habari kushambuliwa kikatili na hata wakati mwingine kuuawa hapa Tanzania.

Bado tunakumbuka matukio ya hivi karibuni ya kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi, mkoani Iringa na Issa Ngumba wa Radio Kwizela mkoani Kigoma.

Kadhalika, tunakumbuka kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwa Mhariri wa gazeti la Business Times, Mnaku Mbani.

Matukio haya hadi leo yamebaki kuwa kitendawili kilichokosa mteguaji kwani haieleweki nini msukomo wake na kuweka wingu zito katika tasnia ya habari nchini kama ni sehemu salama ya kufanyia kazi au kuna hujuma za makusudi zinazofanywa dhidi yao kutokana na kazi yao ya kuuhabarisha umma.

Tunaunga mkono hatua zilizotangazwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), kuwa watafanya uchunguzi ili kupata chanzo halisi cha tukio hilo  na kutoa taarifa kwa umma ili ukweli ujulikane.

Si nia yetu kumtupia lawama au tuhuma mtu yeyote kwa sasa kuhusiana na tukio hilo kwani bado ni mapema na haijathibitika nani aliyehusika.

Hata hivyo, mazingira ya tulio lenyewe lilivyotokea, yanaonyesha wazi ni jambo la kupangwa kwa malengo maalum.

Tunasema hivyo kwa sababu kama lingekuwa ni tukio la ujambazi wa kawaida, wahusika wasingeacha kubeba vitu vya thamani kama kompyuta na vifaa vingine vilivyokuwamo ndani ya gari lake.

Badala yake, watu hao walitoweka baada ya kutimiza lengo lao la kumdhuru Kibanda.

Ndiyo maana tunasema tukio hilo halipashwi kuchukuliwa kijuujuu na kufumbiwa macho ili upepo upite,  tunataka kuona weledi wa vyombo vya dola katika uchunguzi tena kwa haraka na taarifa kutangazwa kwa umma.

Tunataka kuona haki inatendeka kwa wahusika kutiwa mbaroni na kufikishwa mbele ye vyombo vya sheria.

Tunaungana na waandishi wa habari nchini na wanafamilia kumpa
pole Kibanda kwa masaibu yaliyomkuta Kibanda.

Hata hivyo, matarajio yetu makubwa ni kuona uchunguzi wa kina na wa haraka unafanyika kuwabaini wahusika na kitendo hiki kisicho na chembe ya ustaarabu.

Aidha, hatutarajii kusikia kauli za vyombo vya dola kuwa uchunguzi unaendelea bila kuona maendeleo yoyote ya wahusika kutiwa nguvuni na mwisho wa siku jambo hili life taratibu na kusahaulika kama mengine yaliyotokea siku za nyuma.

 

SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles