Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Necta: Waliofeli wameendelea kufeli

27th March 2013
Print
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya awamu ya kwanza ya wanafunzi waliofeli mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana na kukata rufaa kuomba kusahihishiwa upya huku yakionyesha kuwa wanafunzi 530 matokeo yao yamebaki kama yalivyokuwa awali.
 
Matokeo ya wanafunzi hao yamebaki kama yalivyokuwa awali yalipotangazwa Februari 18, nwaka huu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
 Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyowekwa kwenye tovuti ya Necta, wanafunzi 537 walikata rufaa kwa Necta na kusahihishiwa upya mitihani yao. 
 
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, wanafunzi 537 matokeo yao hayajabadilika bali yamebaki kama yalivyokuwa awali.
 
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi sita matokeo yao yamebadilika kutoka alama F na kuwa D na mwanafunzi mmoja aliyepata alama D matokeo yake yamebadilishwa na kuwa alama F.
 
Ofisa Habari na Uhusiano wa Necta, John Nchimbi, akizungumza na NIPASHE jana alisema utaratibu uliopo ni kwamba mwanafunzi anatakiwa kukata rufaa ndani ya miezi miwili tangu matokeo hayo kutangazwa.
 
Nchimbi alisema matokeo yaliyotangazwa ya wanafunzi waliokata rufaa ni ya awamu ya kwanza na kwamba mwisho wa kupokea rufaa hizo ni Aprili 18, mwaka huu.
 
“Necta inaendelea kupokea rufaa nyingine hivyo taarifa za kwamba wanafunzi waliokata rufaa ni 10,000 na kwamba wamefeli zaidi siyo sahihi,” alisema Nchimbi. 
 
 NIPASHE jana ililipoti kuwa wanafunzi waliokata rufaa kutaka mitihani yao isahihishwe upya ni 10,000 na kwamba wamefeli zaidi baada ya kusahihishiwa.
 
NIPASHE ilikuwa imeandika habari hizo ikikariri vyanzo vya ndani ya NECTA na wizarani juu ya kufeli zaidi kwa watahiniwa hao.
 
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, juzi akizungumza na NIPASHE alisema kuwa mitihani ya wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 mwaka huu.
 Dk. Ndalichako alisema hata hivyo, hakuwa na taarifa kama matokeo ya wanafunzi hao yanaonyesha kuwa wengi wamefeli zaidi kwa kuwa alikuwa safarini kikazi.
 
 Alisema suala la kufeli zaidi wanafunzi waliokata rufaa linawezekana kutokea kwa sababu kila mwaka imekuwa ikijitokeza hali kama hiyo, hivyo ni jambo la kawaida.
 
 Matokeo ya mtihani huo uliofanyika mwaka jana nchini yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 (asilimia 60.6) walipata sifuri, huku 23,520 (asilimia 5.16) ndiyo waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza, la pili na la tatu.
 
Watahiniwa 103,327 (asilimia 26.02) walipata daraja la nne ambalo halitofautiani na sifuri kwa kuwa siyo rahisi kwa mhitimu kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika vyuo.
 
Jumla ya watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.
 
Watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.
Kutokana na matokeo hayo kuwa mabaya, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliunda tume kuchunguza chanzo cha kushuka kwa matokeo hayo.
 
Timu hiyo Mwenyekiti wake ni  Profesa Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Makamu Mwenyekiti, Bernadetha Mushashu ambaye ni  Mbunge wa Viti Maaulm (CCM) Mkoa wa Kagera.
 
Mjumbe mwengine ni Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ambaye alikataa uteuzi na kusema ni sawa na kulamba matapishi yake kwa kuwa alikuwa na mgongano na serikali juu ya hoja yake binafsi kuhusu mitalaa ambayo iliporwa kiaina bungeni na serikali.
 
Wengine ni Abdul Malombwa, Profesa Mwajabu Possi, Honorath Chitanda, Daima Matemu, Mahamoud Mringo na Rakeshi Rajan.
 
Wengine ni Peter Maduki, Mwalimu Nurdin Mohamed ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Alharamain, Suleiman Hemed Khamis, Abdalla Hemed Mohamed Mabrouk, Jabu Makame kutoka Baraza la Elimu Zanzibar na Kizito Lawa kutoka Taasisi ya Kukuza Mitalaa.
 
Hivi sasa timu ya Pinda inaendelea kukusanya maoni katika mikoa ya Visiwani baada ya kukamilisha kazi hiyo katika mikoa tisa ya Bara. 
 
Tayari timu hiyo imetembelea mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Manyara, Arusha, Lindi, Shinyanga, Simiyu, Mtwara na Tanga.
 
 
SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles