Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbunge afariki dunia

29th March 2013
Print
Baadhi ya wabunge na wananchi wakiwa nje ya Msikiti wa Muhimbili jijini Dar es Salaam kufuatilia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Chambani, Zanzibar, aliyefariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana.

Mbunge wa Jimbo la Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis, ambaye aliugua ghafla juzi wakati akihudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, amefariki dunia.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa, ndiye alikuwa wa kwanza kutoa taarifa ya msiba huo kwa wajumbe wa kamati yake wakati wakipitia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) jana.

Kwa masikitiko na majonzi, Lowassa alimkatisha Mbunge wa Kikwajuni (CCM), Hamad Yusuf Masauni, aliyekuwa akizungumza na kueleza kwamba: “Naomba nikukatishe Mheshimiwa, ni kwamba mwenzetu hatunaye tena, ametutoka.”

Alisema jana asubuhi, yeye (Lowassa) na Makamu wake, Mussa Azzan Zungu, walikwenda kumtembelea hospitalini na hali yake haikuwa nzuri kwa kuwa alikuwa chumba cha uangalizi wa madaktari (ICU), akiwa hana fahamu.

Alisema baada ya kufanyiwa uchunguzi juzi, madaktari walibaini kwamba alipata shinikizo la damu lililosababisha kupata kiharusi na mshipa mmoja wa damu wa kichwani kupasuka.

“Leo (jana), tumekwenda kumjulia hali, presha ilikuwa imeshuka sana na madaktari walitueleza kwamba wasingeweza kutibu majeraha ya kichwani hadi hapo presha itakapokuwa sawa, lakini kwa bahati mbaya ametutoka mchana huu,” alisema.

Wabunge walipokea kwa mshtuko taarifa hiyo na Lowassa aliwataka wasimame kwa dakika moja ili kumwombea mwenzao na aliahirisha kikao na kutangaza kupitisha bajeti ya EAC akieleza kwamba wataichambua kipengele kwa kipengele mjini Dodoma kabla haijawasilishwa Bungeni.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alithibitisha taarifa za msiba huo akieleza kwamba shinikizo la damu lilisababisha kupasuka kwa mshipa wa damu kichwani hali iliyofanya damu kuingia kwenye ubongo.

Alisema Bunge jana lilikuwa linaandaa utaratibu wa kumsafirisha marehemu kwenda Chambani Pemba kwa maziko na kwamba wabunge 12 wataliwakilisha Bunge kwenye msiba huo.

Hata hivyo, alisema Lowassa na Zungu ni baadhi ya wabunge wanaojiandaa kwenda Chambani kwenye maziko.

Alisema mbunge huyo aliugua kwa muda mrefu mwaka jana na alitibiwa nchini India na kupata nafuu, lakini juzi aliugua ghafla akiwa kikaoni.

Joel alisema kutokana na msiba huo, shughuli za kamati za Bunge zimehairishwa hadi Jumanne Aprili 2, mwaka huu.

“Marehemu ataagwa leo saa 2:30 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na kusafirishwa kwa ndege kwenda Pemba saa 4:00 asubuhi na mazishi yake yatafanyika jimboni kwake majira ya mchana, Spika Anne Makinda, anatoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Chambani, wajumbe wa kamati, wabunge na Watanzania wote,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

SALAMU ZA MBOWE

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na kwamba wamemteua Mbunge wa Mpanda, Said Amour Arfi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwasiliana na uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kujua walivyojipanga.

“Msiba ni wetu sote hatufuati utaratibu wa kivyama bali wa Bunge, kwa kuwa mbali na tofauti za kichama, lakini ni mwezetu kwa maana ya mwakilishi wa wananchi na kila mtu lazima akumbwe na mauti bila kujali chama au dini, lazima tushirikiane katika safari ya mwisho ya mwenzetu,” alisema Mbowe.

SITTA: NI PIGO

Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samueli Sitta, alisema Bunge limepata pigo kwa kuwa ni mmoja wa wabunge wa siku nyingi tangu Bunge la tisa na alibobea katika sekta ya kilimo, kila wakati wa kikao cha Bunge alikuwa akiuliza maswali yanayohusiana na sekta hiyo.

“Kifo hiki ni ghafla sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa,” alisema Sitta.

CUF jana kilitoa taarifa kuhusiana na kifo cha mbunge huyo.

Abdual Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF, alisema: “Uongozi wa CUF unawapa pole wananchi wote, wanachama wa CUF na hasa wananchi wa Jimbo la Chambani kwa kuondokewa na mbunge wao kipenzi. Chama kipo pamoja nao katika wakati mgumu wa kumsindikiza mwenzetu."

JK ATUMA SALAMU

Rais Jakaya Kiwete ametuma salaam za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, na CUF kufuatia kifo cha Khamisi.

Taarifa ya Rais kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa:

“Nimesikitishwa sana na kifo cha Mheshimiwa Salim Hemed Khamis, kifo chake kimetokea wakati ambao Bunge linamhitaji na wananchi wake wa Chambani kuwawakilisha katika vikao vya Bunge vinavyotarajia kuanza Aprili 9 kwa umakini mkubwa.”

Alimuelezea marehemu kuwa aliwatumikia wananchi wake hadi dakika ya mwisho na kwamba ametimiza wajibu wake kwa moyo wote bila kukosa.

Aliwaomba wabunge wenzake na wananchi wake kumuombea kwa mwenyezi Mungu pumziko la milele.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

Articles

No articles