Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Bunge kama vita

18th April 2013
Print
  Lissu, Lema, Wenje, Sugu, Msigwa, Kiwia wafukuzwa
Naibu Spika, Job Ndugai.

Kulikuwa na kila dalili kwamba kikao cha jana cha Bunge kisingemalizika kwa amani kutokana na misimamo mikali baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) juu ya hotuba ya Waziri Kivuli wa Kambi ya Upinzani katika Ofisi ya Rais, baada ya hotuba hiyo kupingwa na wabunge wa CCM na mawaziri kadhaa kwa maelezo kuwa kilichoandikwa katika kurasa nne za mwanzo zinaingilia uhuru wa mahakama.

Wakati suala hilo lilitatuliwa kwa kukutana kwa kamati ya Bunge ya Kanuni, hali katika kikao cha jioni ilikauwa mbaya kiasi cha kuamsha joto baya ambalo lilimfanya Naibu Spika, Job Ndugai, kuamua kumtoa nje ya Bunge mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, kutokana na kuendelea kusimama mfululizo kutaka kupewa fursa ya kumpa taarifa Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, aliyekuwa azingumzia suala la udini akilifungamaisha na Chadema.

Lissu alisimama kutaka kutoa taarifa, lakini Ndugai alimtaka akae chini na kuwa mvumilivu kuwasilikiza wengine kwani hata kama ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani anapaswa kujifunza kuwasililiza wengine na kwamba alikuwa amekwisha kusimama zaidi ya mara 20 katika kikao cha jana.

Lissu aliendelea kusimama na Ndugai akaamua kuita askari ili kumtoa nje, lakini wabunge wengine wa Chadema, Ezekiel Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Godbless Lema (arusha Mjini) waliingilia kati kuzuia Lissu kutolewa.

Kwa kitendo hicho, Ndugai aliwaita askari wengine zaidi kumuondoa Lissu kisha akatoa uamuzi wa kuwafukuzwa bungeni na wamepewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano mfululizo kuanzia leo.

Msuguano wa jana ilianza kuonyesha dalili kwamba siku isingemalizika salama kwa sababu hotuba ya kambi ya upinzani iliyokuwa isomwe na Waziri Kivuli, Profesa Kulikoyela Kahigi, iliibua mvutano mkubwa.

Propfesa Kahigi ambaye pia ni mbunge wa Meatu kupitia Chadema, alikuwa asome hotuba hiyobaada ya Mawaziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Celina Kombani (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Stephen Wasira (Mahusiano na Uratibu), pamoja  na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, kuwasilisha  hotuba zao.

Kilicholalamikiwa ni maelezo yaliyomo kwenye ukurasa wa kwanza hadi wa nne wa hotuba hiyo.

Awali Ndugai, alimwita Profesa Kahigi kuwasilisha hotuba, lakini muda mfupi baada ya kuanza kusoma, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisimama na kuomba mwongozo akisema ukurasa wa kwanza hadi wa nne wa hotuba hiyo unaingilia uhuru wa mahakama.

Alimtaja Mbunge wa Chadema, Mustapha Akunaay (Mbulu), kuwa alitoa angalizo likakubaliwa bungeni kwamba masuala yaliyoko mahakamani yasijadiliwe.

Serekumba aliyataja mambo yaliyoko kwenye kurasa hizo kuwa yanahusu Usalama wa Taifa, kesi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare.

Maoni yake yalipingwa na ufafanuzi wa Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

MNYIKA
Maelezo yaliyo kwenye ukarasa wa kwanza hadi wa nne hayagusii kesi zilizoko mahakamani. Kinachotajwa ni kiapo cha Dk. Ulimboka, kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi na kazi za Usalama wa Taifa.

LUKUVI

Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipinga maelezo ya Mnyika akieleza kuwa sheria ya Usalama wa Taifa inakataza kutaja majina ya watumishi wa idara hiyo.

Alisema katazo lipo kwenye kifungu cha 16 cha sheria hiyo na pia kukiuka kanuni ya 64 (c) ya Bunge inayozuia kuingilia uhuru wa mahakama.

NDUGAI
Ndugai alitoa angalizo kuwa kinachoonekana ni kuingilia uhuru wa mahakama kwa kurejea kesi zilizoko mahakamani kama ilivyotokea kwenye hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Freeman Mbowe iliyosomwa wiki iliyopita.

Alikumbushia kuwa Spika, Anne Makinda, aliwaonya wabunge kuwa kesi hizo zisijadiliwe tena bungeni. Ndugai aliushangaa upinzani kwa kurudisha mambo yaliyozuiliwa.   

HALIMA MDEE
Baada ya hapo Halima Mdee (Chadema) Kawe, alisimama na kueleza kuwa kurasa hizo hazikurejea kesi ya Lwakatare na ukurasa wa nne unalitaja jina lake bila kuzungumzia mwenendo wa kesi, ila unaelezea taratibu za kukamatwa kwake.

“Hoja zinazoletwa na Mheshimiwa Lukuvi zitaje vifungu vya sheria ya Usalama wa Taifa vinasemaje ili tulinganishe na kile tulichokiandika hapa. Kilichoandikwa hakuna jipya yanajulikana, ndiyo maana tunaleta mbele ya Bunge lako ili serikali ichukue hatua,” alisema.

TUNDU LISSU
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema maelezo yanayotolewa bungeni na mnadhimu ni mambo ya kuokoteza mitaani hayapo katika sheria ya Usalama wa Taifa anaouzungumzia.

Alisema kinachokatazwa ni majina ya watumishi wa idara hiyo kwenye magazeti, televisheni ama kwenye matangazo.

Alisema idara hiyo inaongozwa na Mkurugenzi ambaye anapewa maelekezo na Waziri anayewajibika kwa Bunge hivyo kulikataza Bunge lisijadili utendaji mbovu wa taasisi ambayo inapata fedha kupitia kodi za wananchi ni jambo lisilokubalika.

“Hakuna kesi iliyotajwa hapa nadhani wengi hawaelewi kipengele cha makatazo kinachozuia kuzungumzia ushahidi wa kesi unaotolewa mahakamani,” alisema na kuongeza:
"Kama  hotuba hii inazungumzia ushahidi nitakuwa mtu wa kwanza kuunga mkono kurasa hizo ziondolewe vinginne kama hakuna ushahidi unaotajwa ni kuziba mdomo Kambi ya Upinzani Bungeni na litakuwa jambo la hatari ambalo halitakubalika.”

NAIBU WAZIRI SHERIA
Naibu Waziri Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alipinga ufafanuzi huo.

SERUKAMBA

Baada ya maelezo hayo, Serukamba alisimama tena na kusisitiza kuwa haiwezekani wabunge waje bungeni kujadili kesi zilizoko mahakamani akitaja shauri la Lwakatare ambalo lipo kortini.

OLE SENDEKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema ukurasa wa nne wa hotuba ya Kambi ya Upinzani unataka mtu aliyeghushi mkanda wa tuhuma zinazomhusu Lwakatare achukuliwe hatua hivyo kuamua kama kuna kughushi au lah ni kazi ya mahakama na siyo Bunge.

MAAMUZI YA SPIKA
Baada ya mjadala huo uliotawaliwa na jazba, Ndugai aliagiza Kamati ya Kanuni kujadili na kushauri hatma ya hotuba hiyo.

Alisema kwa vile inahusu kanuni ndiyo maana aliamua kuiagiza kamati hiyo kulijadili na kuwasilisha majibu katika kikao cha jana jioni.

Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Chana akisoma maoni  ya kamati hiyo, Mnadhimu Lukuvi, alikuwa akihangaika kushauriana na viongozi wa serikali na wabunge wa CCM juu ya hotuba hiyo.

Aliwasiliana na wabunge William Ngeleja (CCM), Sengerema na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.

LEMA ALIPUKA
Wakati wa jioni, mbunge ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu,  Godbless Lema, alitema cheche bungeni akikitaja Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa dicho kinaasisi siasa za udini nchini.

Aliliambia Bunge jana akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma na ile ya Mahusiano na Uratibu.

Alisema na kusisitiza kuwa nchi imegawanyika kutokana na  mgogoro wa dini na waasisi ni CCM ambayo ni mwasisi wa siasa za ubaguzi wa kidini na kikabila.

Kutokana na maelezo hayo, Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais, William Lukuvi alimtaka Lema kufuta kauli hiyo au kuithibitisha kwa kuwa ni dhihaka.
Licha ya Lema kuondoa kauli hiyo alisema yeye hana cha kufuta bali kuongeza msisitizo na kueleza kuwa CCM iliasisi udini pale ilipoanza kueneza imani kuwa CUF ni chama cha Waislamu; na pale Chadema ilipofanya vizuri CCM ilianza tena kusema kuwa Chadema ni chama cha Wakristo na cha kikanda.

Alisema anahofia kukatwa kucha, kung’olewa meno na kope za macho yake ambazo usalama wa taifa unaweza kuzing'oa kwa kutumia koleo.

Alikataa kufuta kauli hiyo na kulieleza Bunge kuwa, Waziri Lukuvi ndiye anayefanya siasa za ubaguzi wa kidini.

Aliongeza kuwa Lukuvi anaangalia wadhifa wake kama ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na madaraka mengine, lakini haangalii mustakibali wa taifa. Alieleza kuwa kuthibitisha kuwa anaendeleza siasa za udini na kupuuza kuzungumzwa jambo hilo alimwambia Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kuwa hizo kanda za chuki za udini za Chuo Kikuu cha Dodoma alizowasilisha bungeni ni za Chadema.

“Hapa sina kauli ya kufuta labda ni kusisitiza"
Jumatatu Selasini aliwasilisha kanda zinazoeleza jinsi chuo hicho kilivyojaa chuki za kidini wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Lukuvi alikanusha maelezo ya Lema na kueleza kuwa hakuzipokea kanda hizo ila Katibu wa Bunge alimwambia Selasini kama hajatia saini  hazitapokelewa kwenye Ofisi ya Bunge.

MWANASHERIA MKUU
Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, alisimama na kuliambia Bunge kuwa Lema anasema mtu ambaye ni kinara wa mambo ya udini ni Rais na kumuomba athibitishe ama afute kauli hiyo inayokwenda kinyume na Kanuni ya 64 (1)(D) inayokataza kutumia jina la Rais kwa dhihaka.

LISSU NIni MAANA YA DHIHAKA?
Lissu alisimama na kutoa maelezo kuwa Kanuni hiyo inakataza kutumia jina la Rais kwa dhihaka lakini haikatazi kumkosoa Rais.

Alisema neno dhihaka ni mambo ya kiutani utani mfano Rais msanii lakini kusema kuwa akitumia neno  ‘anaasisi’  ni kauli nzito na maneno makubwa lakini siyo dhihaka.

“Kanuni haijasema Rais asiokosolewe, labda tubadilishe kanuni kuondoa dhihaka tutumie neno ‘kumsema Rais vibaya.”

Kwa msimamo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alimwomba Lema athibitishe kauli zake.

Lema aliliambia Bunge kuwa yuko tayari kuthibitisha na akapewa siku saba na Ndugai kufanya hivyo.

Hata hivyo, Lissu na wabunge wenzake wamesema leo wataingia bungeni kama kawaida kwa kuwa hakuna kanuni inayomzuia mbunge kuomba mwongozo, utaratibu au kutoa taarifa.

Lissu amesema kanuni zinaeleza kwamba kama Spika anataka kumfukuza mbunge kwa muda mrefu ni sharti asikilizwe nafasi ambayo hawajapewa.

SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles