Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Dkt. Slaa aingia jimboni kwa Makinda

27th April 2013
Print
Dk.Wilbrod Slaa

Wakazi wa Jimbo la Njombe Kusini, wanaoongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, wamemweleza Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Wilbrod Slaa kwamba pamoja na chama hicho kukusanya saini za wananchi ili kulipa bunge ‘meno’ ya kuitaka serikali ipunguze ongezeko la kupaa kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei nchi, Makinda amepunguza kasi ya kulitembelea jimbo hilo.

Dk. Slaa alifika katika jimbo hilo jana akiongozana na wabunge wa chama hicho waliopewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya bunge wiki iliyopita na kuamua kuzunguka mikoani kukishitaki kiti cha Spika na Naibu wake Job Ndugai kwa kutoa adhabu hiyo.

Spika Makinda alibariki adhabu iliyotolewa na Naibu wake, Job Ndugai dhidi ya wabunge sita wa Chadema ambao ni Mnadhibu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Ezekia Wenje (Nyamagana),Hyness Kiwia (Ilemela), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini).

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa NHC mkoani hapa, wananchi hao (Hawakutaka kutajwa majina yao), walimweleza Dk. Slaa kwamba Spika Makinda hajafanya ziara za mara kwa mara katika jimbo hilo jambo ambalo linawafanya wao kwamba kiti cha spika kimemzidi.

“Haonekani mara kwa mara hapa jimboni na hii inatufanya tuone kama kiti kimemwongezea majukumu hadi anasahau kwamba yeye ni mbunge, kwa hiyo tunaomba muwe karibu na sisi, msije tu wakati mnapofukuzwa bungeni, hebu mje mara kwa mara,” alisema.

Kutokana na madai hayo ya wananchi, Dk. Slaa aliwahoji wananchi hao kama wanachofanya wabunge sita wa Chadema ambao wamepewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya bunge kwa siku tano ni sahihi na kwamba anataka kufahamu ni mara ngapi mbunge wao (Makinda) amefika kuwatembelea jimboni.

"Tumemuona wakati alipokuja kushukuru baada ya kupata ubunge ila wakati mwingine huwa tunasikia kuwa yupo jimboni akizungumza na wananchi," alisema mmoja wa wananchi hao.
Baada ya swali hilo, Dk. Slaa alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitafuta mchawi wa huku ikitumia propaganada kuwa Chadema ni chama chenye migogoro badala ya kuangalia maisha ya Watanzania wanaoishi kwa kula kwa tabu.

"Nawaambieni wananchi wa Njombe Kusini kuwa, propaganda zinazotolewa na serikali yenu kuwa Chadema ina migogoro ni uongo mtupu. Chadema haina migogoro wala haijawahi kuwa na migogoro. Hizo ni propaganda za mtu anayeshindwa hoja na kutetea watu wake waliomtuma kuwawakilisha" alisema Slaa.

Aliwataka wanachi wa jimbo hilo kuwa makini na viongozi amabo hawawajibiki kwao na badala yake wamekuwa wakitafuta maslahi yao binafsi pasipo kujali umma uliowachagua.

Katika mkutano huo, wakazi wa jimbo la Njombe Kusini walichanga zaidi ya Sh. 700,000 kwa ajili ya kuwaunga mkono wabunge hao katika kuelezea yaliyotokea bungeni wiki iliyopita na kusababisha kupewa adhabu ya siku tano kutohudhuria vikao vya bunge. 

SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles