Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Dawa za kupunguza unene zampotezea uhai

27th April 2013
Print

Mwanamke mmoja amepoteza maisha baada ya kunywa dawa zinazodaiwa kuwa ni za kupunguza unene kufuatia kuharisha na kutapika mfululizo, jijini Dar es Salaam.

Marehemu huyo (jina linahifadhiwa) alifariki dunia Ijumaa wiki iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam akidaiwa kunywa dawa za kupunguza tumbo zinadaiwa kutoka Uarabuni na kusababisha kuharisha hadi kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu.

Ndugu wa karibu wa marehemu, aliiambia NIPASHE Jumamosi kuwa ndugu yake alikunywa dawa hizo kwa ajili ya kupunguza tumbo.

Alisema hata hivyo baada ya kunywa dawa hizo hali yake ilibadilika ghafla baada ya kuanza kuharisha na kutapika na kuamua kumpeleka Hospitali ya Dar Group eneo Tazara.

Alisema kuwa siku mbili kabla ya kunywa dawa hizo alikuwa akisita kuzinywa na kwamba siku iliyofuata baada ya kula chipsi mchana ndipo alipoona tumbo lake limejaa gesi na kuamua kutumia dawa hiyo kwa ajili ya kupunguza tumbo.

"Alijua tumbo lilivyojaa akinywa hizo dawa ndipo ataharisha matokeo yake amejikuta akijisikia vibaya zaidi," alisema.

Alisema baada ya kunywa hali yake ilianza kubadilika na kuamua kumpeleka katika hospitali hiyo ambako alitundikiwa dripu za maji pamoja na kuwekewa oxygen baada ya hali yake kubadilika.

Hata hivyo, alisema hali ya mgonjwa huyo iliendelea kuwa mbaya na siku iliyofuata alipewa rufaa kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Alisema kuwa mgonjwa huyo alilazwa katika wodi ya Mwaisela na ameacha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

NIPASHE Jumamosi ilifika katika Hospitali ya Dar Group na kufanikiwa kuzungumza na Dk. Restuta Kibasa ambaye alimhudumia mgonjwa huyo.

Dk. Kibasa alisema mgonjwa huyo alikuwa akiharisha pamoja na kutapika vitu vya kijani na kwamba wazazi wake hawakuwa wakweli kueleza kilichokuwa kinamsumbua mgonjwa zaidi ya kueleza kwamba alikula chipsi.

"Sasa wanasema amekula chipsi matapishi anayoyatapika hayaendani na hiki tunachoelezwa mara wakati mwingine nikawasikia ndugu zake wakisema amekunywa dawa za suna ambazo mimi sizifahamu," alisema Dk. Kibasa
Dk. Kibasa alisema mgonjwa huyo walimtundikia dripu za maji baada ya kushindikana kunywa dawa kutokana na kutapika mfululizo.

Alisema hali yake iliendelea kuwa mbaya kiasi cha kupoteza fahamu ndipo walimpa rufaa na kwenda hospitali ya Muhimbili.

Hata hivyo, Dk. Kibasa alisema pamoja na kwamba hafahamu sana kuhusu dawa za asili zinazopunguza unene, kitaalamu suala la kupunguza mwili kwa haraka linaharibu mfumo mzima wa mwili wa binadamu.

Alisema kupunguza mwili kwa ghafla kunaweza kuleta madhara makubwa kwa mtumiaji wa dawa hizo kwa kuwa mfumo wa damu pamoja na mwingine wote wa mwili huvurugika.

Alisema kitaalamu inashauriwa kwamba, mtu akitaka kupunguza uzito afanye hivyo taratibu ikiwamo kupunguza kula na kufanya mazoezi na sio kutaka kupungua kwa haraka. 

SOURCE: NIPASHE

Articles

No articles