Monday Feb 8, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wananchi wapewa somo la ardhi

10th May 2013
Print
Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye.

Serikali imetoa wito kwa wananchi kutouza ardhi yao kwa wawekezaji wa nje wala wa ndani na badala yake waitumie kama mitaji yao kwa kuingia ubia na wawekezaji husika.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye, alitoa changamoto hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na ujumbe wa wabunge wa Kamati ya Mazingira ya Ujerumani, iliyopo nchini kwa ziara ya kikazi.

Alisema kwa mujibu wa Sera ya Ardhi ya mwaka 2011, Watanzania wana fursa ya kushiriki uwekezaji wa kila aina unaofanywa kwenye ardhi na kwamba wametengewa asilimia 25 ya hisa.

"Ni lazima wananchi au serikali iwekeze kwa niaba ya wananchi kwenye kila uwekezaji uwe hoteli, kilimo kikubwa au kiwanda," alisema.

Alisema ni kwa msingi huo pekee utakaoweza kuwanufaisha wananchi na taifa kutokana na uwekezaji unaofanyika nchini.

"Akija mtu akitaka shamba la kulima, usimuuzie mwambie mlime wote hata kama huna mtaji wa fedha, ardhi ndiyo iwe mtaji wako...msifanye hivyo tu kwa wawekezaji wa nje, bali hata wa ndani," alisema Medeye.

Alisema kwa kuanzia, serikali itafanya hivyo kwenye ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni na kwamba mfuko maalumu umeanzishwa kwa ajili ya kuuza hisa kwa wananchi na kwamba kipaumbele kitakuwa kwa wananchi wa eneo hilo.

Ujumbe wa wabunge hao wa Ujerumani, umeongozwa na Joseph Goppel. Wengine ni Dorothea Steiner, Marco Burrow na Sabine Ursula Stuber.

Wabunge hao wameweka msisitizo katika suala la utunzaji wa mazingira hasa ardhi oevu na mgawanyo wa rasilimali za maji.

SOURCE: NIPASHE