|
PPT-Maendeleo kupokea watakaobwagwa kwenye kura za maoni
2005-07-22 15:09:28
Na Joseph Mwendapole, Jijini
Chama cha upinzani cha PPT-Maendeleo kimesema kiko tayari kuwapokea wanasiasa watakaobwagwa na vyama vyao kwenye kura za maoni.
Tunawakaribisha na tutawapa nafasi wajaribu bahati yao,amesema Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Peter Mziray.
Amesema PPT Maendeleo imejiwekea mkakati maalum wa kushinda nafasi za udiwani na ubunge na kwamba wanatoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kuomba nafasi hizo mapema.
Aidha amesema safari hii amekuja na nguvu mpya ya kumgoa kwenye nafasi ya ubunge wa jimbo la Same Mashariki mgombea yoyote atakayesimamishwa na CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akasema hivi sasa amejiandaa vya kutosha na anachosubiri ni kumwona mteule wa CCM ambaye atambwaga.
Bw. Mziray akadai kuwa hata mwaka 2000 alimtoa jasho mgombea wa CCM, Bw. Daniel Yona ambaye ni mbunge na Waziri wa Nishati na Madini na kwamba alishinda kutokana na mizengwe tu ya chama hicho.
Amesema kuwa ndani ya CCM kuna wagombea tisa wanaowania kuteuliwa kugombea jimbo hilo na lakini akatamba kwamba hakuna mwenye ubavu wa kupambana naye kwa kuwa wananchi wa jimbo hilo wamechoshwa na ahadi hewa za CCM.
Akasema atapata mteremko endapo chama hicho kitamsimamisha mbunge wa sasa Bw. Daniel Yona kwa kuwa wananchi wa jimbo hilo wamemchoka na wanamsikia kwenye redio tu.
Akasema ameamua kuwania tena nafasi hiyo licha ya kuanguka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 kutokana na maombi ya wananchi walio wengi wa jimbo hilo.
Wameniomba nimwondoe Yona endapo atasimamishwa na CCM kwa kuwa wamechoka kuahidiwa ahadi ambazo hazitekelezeki,akatamba.
Kuhusu uamuzi wake wa kuacha kuwania nafasi ya Urais, akasema ameshauriwa na wazee wa jimbo hilo kuachana na nafasi hiyo na badala yake awanie ubunge ili awawakilishe vyema bungeni.
|