|
Waislam kuandamana
2005-07-22 15:13:13
Na Badru Kimwaga, Jijini
Waumini wa Dini ya Kiislam Jijini Dar es Salaam leo mchana wanatarajiwa kufanya maandamano makubwa kwa ajili ya kuhamasishana juu ya uchaguzi mkuu wa Wabunge na Rais unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu.
Maandamano hayo yataanzia meeneo ya Mnazi Mmoja na kumalizikia viwanja vya Bakhresa-Manzese, ambapo utafanyika mkutano wa hadhara utakaotangaza chama na mgombea anayefaa kuchaguliwa kwa urais.
Kwa mujibu wa vipeperushi vilivyobandikwa katika misikiti kadhaa na katika maeneo mengine ya Jijini, maandamano hayo yameandaliwa na Kamati ya Shura ya Maimamu nchini kupitia Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislam (BARAZA KUU).
Maandamano hayo yatafahamika kama Waislam na Uchaguzi Mkuu wa 2005 na yatapitia katika mitaa ya barabara ya Bibi Titi Mohammed, Morogoro njia ya Jangwani, Magomeni na kisha kuishia pale Manzese.
Mara maandamano hayo yatakapofika katika viwanja hivyo vya Bakhresa kutakuwa na mkutano mkubwa ambao utahutubiwa na masheikh mbalimbali maarufu wa dini hiyo akiwemo Amir Mkuu, Sheikh Mussa Kundecha.
Masheikh wengine wanaotarajiwa kunguruma katika mkutano huo wa kuwatangazia waumini wao yupi na chama gani kinachofaa kupigiwa kura kwa ajili ya kushika madaraka ya nchi ni Sheikh Issa Ponda, Jumanne Amri, Said Ricco na wengineo ambao wapo katika harakati za kuutanza uislam.
Ni muhimu kwenu Waislam kushiriki katika maandamano na kuhudhuria mkutano huo ili kuweza kupewa mkakati wa kumtambua mgombea anayefaa kupigiwa kura kwa ajili ya urais wa awamu ya nne,sehemu ya vipeperushi hivyo inasomeka.
Maandamano hayo yanatarajiwa kuanza mara baada ya swala ya Ijumaa majira ya saa 7:30 na mkutano huo utaanza saa 9 alasiri na kumalizika saa 12 jioni.
|