|
Maiti yazua kizaazaa
2005-07-22 15:13:48
Na Asha Kigundula, Magomeni
Sakata la kugombea maiti ambalo limekuwa gumzo katika mitaa ya Magomeni Jijini, limeingia katika sura mpya kutokana na kile kilichodaiwa kuwa maiti imeibwa usiku wa manane na kuzikwa kinyemela.
Mwili huo wa marehemu Abubakar Kifunta ulikuwa ukigombewa na pande mbili tangu alipofariki dunia Jumatatu wiki hii.
Soo hilo linahusisha pande mbili zenye madhehebu tofauti, yaani upande wa marehemu pamoja na ule wa mkewe Fatma Ruwamba ambapo kila upande ulikuwa unadai ndio wenye haki ya kuzika mwili wa marehemu.
Wakati ndugu zake walitaka marehemu azikwe kwa taratibu za imani ya Kikristo, mkewe alitaka mumewe azikwe kwa imani ya Kiislam.
Wakati mtafaruku huo ukiendelea, habari za ndani zinadai kuwa upande mmoja ulifanya mbinu na kuuchukua mwili wa marehemu kutoka hospitali ya Mwananyamala ulikokuwa umehifadhiwa na kwenda kuuzika kinyemela.
Habari zaidi zinadai kwamba marehemu alizikwa juzi na ndugu zake kwa taratibu za imani ya Kikiristo katika makaburi ya Mwananyamala.
Shemeji wa marehemu, Bw.Abbas Yusuph amesema mke wa marehemu na familia yake hawakushirikishwa kwenye mzishi hayo.
Kufuatia tofauti hizo, matanga yamewekwa sehemu mbili tofauti, yaani nyumbani kwao Mwananyamala Koma Koma, na nyumbani kwake Magomeni mtaa wa Lalago namba 11.
Licha ya ndugu yao kuzikwa, Bw. Yusuph amesema familia yake sasa imeamua kupeleka suala hilo kortini ili sheria ichukue mkondo wake.
Tunataka suala hilo liamuliwe kisheria. Tukishinda, tutafukua mwili na kuuzika kwa taratibu za Kiislam, akasema Bw. Yusuph.
Kwa mujibu wa Bw. Yusuph, kabla ya kifo chake, marehemu alibadili dini na kuwa Mwislam.
Pia alibadili jina na badala ya kuwa Peter Kifunta akawa Abubakar Kifunta. Anasema alifunga ndoa kwa taratibu za dhehebu hilo katika msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni Mapipa.
Anasema marehemu aliendelea kuwa mwislam hadi alipougua na akiwa hatika hatua za mwisho mwisho za maisha yake ndugu zake wakampa sakramenti.
Marehemu alikuwa dereva wa gari la Raha Leo linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tanga.
Ameacha watoto wawili, Rashid mwenye miaka 11, na Nasra mwenye miaka minane.
|