|
Mwalimu alia sekondari yake mpya kukosa wanafunzi
2005-07-25 14:36:32
Na Moshi Lusonzo, Temeke
Wakati shule kadhaa za Sekondari Jijini zinakabiliwa na tatizo la wingi wa wanafunzi, huko Kigamboni mambo ni tofauti baada ya shule moja iliyofunguliwa karibuni kukosa wanafunzi.
Shule hiyo inayojulikana kama shule ya Abdu Jumbe sasa inakabiliwa na upungufu wa wanafunzi 54 ambao bado hawajaripoti shuleni hapo toka wachaguliwe kujiunga na shule hiyo.
Mkuu wa Shule hiyo Bi Esta Mdachi amewaambia madiwani waliotembelea shule hiyo kwamba mpaka muda huu hajui kwa nini watoto hao hawajaripoti.
Amesema amewapelekea barua ya kuwataarifu kuchaguliwa kwao lakini hawajajibu lolote.
Akasema, kutokana na upungufu huo, imebidi darasa moja kulifunga na kutumiwa matatu pekee.
Waheshimiwa madiwani pamoja na kufunguliwa shule tuna upungufu wa wanafunzi, walioripoti hapa bado ni wachache,akasema.
Akasema idadi inayotakiwa shuleni hapo ni 180, lakini waliopo madarasani ni 126.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo amesema kuwa pamoja na tatizo hilo, pia wana tatizo kubwa la walimu kufuatia walimu waliopelekwa kwenye shule hiyo nao kushindwa kuripoti eneo lao la kazi.
Kutokana na upungufu huo, jitihada zimefanyika kuhakikisha walimu wa ziada wanapatikana, wakiwemo walimu wanaofanya kazi kwa njia ya kujitolea.
Baada ya kilio cha Mkuu wa Shule, diwani wa kata ya Mjimwema, Kapteni Ngasa alionyesha mshangao wa hali ya juu kwani katika maeneo mengine wanafunzi wamekosa nafasi za kusoma.
Diwani huyo aliwaeleza madiwani wenzake kuwa kama suala hilo wangelifahamu mapema juhudi zingefanyika kuwachagua watoto wengine ambao bado wanahangaika mitaani baada ya kukosa nafasi ya kujiunga na masomo ya sekondari.
Madiwani hao walikuwa katika ziara ya siku mbili ya kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya Manispaa yao kabla ya kuachia ngazi mwezi ujao kupisha uchaguzi mkuu.
|