|
Soko ladondoka usiku wa manane
2005-07-25 14:39:20
Na Ally Hengo PST, Kisarawe
Jengo linalotumika kama soko ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa likilalamikiwa kuwa ni bovu, limeanguka usiku na kuharibu bidhaa zilizokuwemo ndani.
Kama jengo hilo lingeanguka mchana, kungekuwa na msiba mzito kutokana na kutumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 40.
Walioshuhudia kizaazaa hicho cha usiku walikuwa ni madereva na makondakta waliolala katika mabasi yao karibu na eneo la soko hilo ambao wamesema walitoka katika magari yao na kutaka kukimbia kutokana na kishindo kikubwa baada ya jengo hilo kudondoka.
Jengo hilo lenye kenchi nene na lililoezekwa mabati ya udongo ya asbestos lilijengwa mwishoni mwa miaka 70.
Kwa kipindi kirefu limekuwa likilalamikiwa na wafanyabiashara kwamba ni bovu na lingeanguka siku yoyote.
Lilidondoka saa tisa wakati likiwa halina watu. Hata hivyo bidhaa zilizokuwemo zimeharibiwa, akasema mmoja wa madereva hao.
Kwa mujibu wa madereva hao, wafanyabiashara walipofika kazini jana asubuhi walistaajabu kukuta kenchi na vipande vya mabati vimelalia meza zilizojengwa kwa simenti.
Madereva hao wamesema kabla ya tukio hilo, kulikuwa na upepo mkali sana.
Hadi juzi, paa ya jengo hilo ilikuwa imebonyea.
Kufuatia hali hiyo, wafanyabiashara hao waliiitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kulifanyia matengezo ili lisije kuleta madhara zaidi, kilio ambacho hakikusikilizwa.
Gazeti hili liliwahi kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kisarawe, Bw. Isamilo Makoye ambaye alisema ofisi yake haihusiki tena na masuala ya jengo hilo.
Alisema miaka ya nyuma lilikuwa chini ya ofisi ya kijiji kabla shughuli za uendeshaji kukabidhiwa kwa chama kilijulikanacho kama CHOBEFA.
Mmoja wa wakurugenzi wa chama hicho, Bw. Method Lugongo naye alipoulizwa kuhusiana na ubovu wa jengo hilo alisema wao hushughulika na masuala ya usafi na kukusanya ushuru na sio masuala ya ujenzi.
Ambapo mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Lewis Kalinjuna ofisini kwake hakuweza kupatikana kwa kile kilichodaiwa kuwa alikuwa kwenye kikao cha madiwani.
|