|
Sitatumia dola kuibeba CCM-Mkapa
2005-07-25 14:41:11
Na Mwinyi Sadallah,Mbweni
Rais Benjamin Mkapa ameahidi kwamba hatotumia vyombo vya dola kuibeba CCM kushinda katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 30, mwaka huu.
Akifungua mkutano wa makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort, Rais alisema kwamba kila chama kitashinda uchaguzi kwa kutumia ubora wa sera zake za kuwavutia wapiga kura.
Akasema kwamba vyombo vya dola havipo kwa ajili ya kukisaidia chama fulani bali kazi yake kubwa ni kudhibiti hali ya usalama tu wakati wote kabla na baada ya uchaguzi mkuu.
Alifahamisha kwamba hakuna chama cha siasa chenye hati miliki ya nchi na hata CCM haina hati miliki na hivyo kina haki ya kushiriki mageuzi ya siasa katika ngazi zote.
Heshima ya chama tawala na heshima ya Tanzania inataka uchaguzi huru na wa haki,akasisitiza Rais Mkapa ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa CCM.
Rais Mkapa akasema kwamba kumekuwa na upotoshaji wa makusudi dhidi yake kwamba atatumia nguvu za dola ili kuibeba CCM katika uchaguzi ujao.
Amesisitiza kwamba vyama vya siasa vitumie sera zake kuwavuta wapiga kura kuwaunga mkono na kuwawezesha kushinda uchaguzi ujao.
Alitahadharisha wananchi wasijaribu kuchagua kiongozi kwa uzuri wa sura bali kwa sera na msingi wa mikakati ya maendeleo kwa maslahi ya taifa na ya watu wake bila ya kujali tofauti zozote zile.
Rais Mkapa aliwaambia wananchi kwamba sifa bora za kiongozi zimwezeshe kutekeleza sera kwa kupitia ilani ya chama chake katika uchaguzi. Sera ziwe kigezo cha mpiga kura kuamua kiongozi gani anafaa kuchaguliwa,akasema katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na Makatibu Wakuu wa vyama vyote vilivyopata usajili wa kudumu.
Akasema kwamba Watanzania watafanya makosa makubwa sana kutanguliza mbele watu wasio na uchungu wa kutosha na amani ya nchi, uhuru, mshikamano na umoja wa kitaifa. Akasisitiza kwamba kiongozi wa nchi lazima aweze kuzingatia misingi ya utaifa na dira ya maendeleo ya taifa.
Aidha Bw. Mkapa alionya kwamba taifa litaangamia mithili ya chombo kisichokuwa na nanga kwenye bahari iliyochafuka endipo kiongozi wa nchi hatoweka mbele utaifa na utekelezaji wa dira ya maendeleo.
Akasema kwamba serikali inajiandaa kuweka utulivu katika uchaguzi na kuwataka watu wote hasa vijana kuepuka kuwasha cheche za mapambano na uhalifu katika kampeni.
Amewataka viongozi wa siasa waepuke kuwachochea vijana kuchafua amani na kupanda mbegu za chuki na uhasama ndani ya nyoyo za vijana wa Tanzania dhidi ya vijana wenzao eti kwa sababu za tofauti za kisisasa.
|