|
Askari akatwa mapanga kanisani
2005-07-25 14:44:25
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili
Katika hali ya kushangaza, askari wa kampuni moja ya ulinzi ya hapa Jijini, amejikuta akikatwa katwa mapanga mbele ya kanisa.
Kwa mujibu wa askari huyo, baada ya kuona wabaya wake wanataka kumuua alikimbilia kanisani kujiokoa lakini bahati mbaya eneo hilo likawa ndio la machinjio yake.
Kutokana na tukio hilo, Mlinzi wa kampuni hiyo inayofahamika kama SG Group Security, Bw. Augustine Mathias, 32,amelazwa katika taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili, MOI, akipatiwa matibabu ili kunusuru maisha yake.
Akizungumza akiwa kitandani kwake, Bw. Mathias akaliambia gazeti hili kuwa tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki iliyopita pale kundi la wapiga debe wa kituo cha Mwenge walipomfanyia unyama huko baada ya kwenda kwenye kituo hicho kwa ajili ya kuwaelimisha juu ya mpango wa Jiji wa kutoa usimamizi katika vituo vya daladala.
Akasema, siku hiyo ya tukio alikuwa ameambatana na wenzake, lakini kabla hawajafika walikwenda ofisi ya serikali ya mtaa na kumchukua mjumbe mmoja ili kutoa usaidizi wakati wakitoa elimu hiyo.
Walipofika katika kituo hicho cha Mwenge, kazi ya kuwaelimisha wapiga debe juu ya utaratibu huo ulianza, na hapo walitumia mtindo wa kuwaelimisha watu wawili wawili ili kuepukana na ghasia kama hawataelewana.
Tulikuwa tunatoa elimu kwa watu wawili wawili chini ya mjumbe yule wa mtaa, na kazi hiyo ilifanywa kwa kupokezana ikiwa watu fulani wanatoa elimu wengine wanakaa sehemu nyingine kuwasubiri ili kujilinda na ghasia, akasema.
Akaongeza kuwa, ilipofika zamu ya wafanyakazi wenzake kutoa elimu, yeye alikwenda kwenye kibanda kimoja akiambatana na wezake na kukaa hapo wakiwasubiri wenzao.
Tulipokaa pale kibandani kwa muda mrefu, tulianza kuingiwa na wasiwasi baada ya kuona wenzetu hawarudi, ndipo tulipoamua kumtuma mwenzetu akaangalie kinachoendelea, akasema.
Kabla mtu waliyemtuma hajarudi, ghafla kundi la wapiga debe liliibuka na kuanza kuwafukuza huku mikononi mwao wameshika mapanga na sime.
Akasema kuwa kwa haraka walitimua mbio hadi eneo la kanisa moja hapo hapo Mwenge na kuingia katika kibanda cha mlinzi ili kujinusuru.
Bw. Mathias akaeleza kwamba baada ya kuingia ndani ya kibanda hicho, walimkuta mlinzi akiwa katika lindo lake na bila kumuuliza chochote walifunga mlango na kulala chini.
Huku mlinzi huyo akiwa amepigwa na butwaa kwa kuingiliwa ghafla, mara kundi la wapiga debe hao walikizunguka kibanda hicho kilichopo kanisani na kumtisha mlinzi awafungulie mlango ili wawatoe watu hao.
Hatukuwa na la kufanya zaidi ya kumuomba mlinzi atupe ulinzi wake ili tunusurike na kifo......hata hivyo nadhani hakutusikia kilio chetu na badala yake alimruhusu mmoja wao kuingia ndani na kuanza kunikata mapanga, akasema huku akionyesha simanzi.
Katika kipigo hicho, panga la kwanza lilimkata vidole vyote na kuviacha vidole hivyo vikininginia, panga la pili likamkata kiwiko cha mkono na la tatu lilimkata nyuma ya kichwa na kuacha damu zikitiririka kila mahali.
Akiwa katika hali mbaya, akasema mara alimsikia mtu huyo akimuita mwenzake kwa jina la Mwenda aingie ndani ya kibanda hicho ili kuwamalizia watu waliobaki.
Nilimsikia akimwita Mwenda! Mwenda! njoo umalizie waliobaki, hapo kwa kweli mimi nilikuwa hoi na hata huyo Mwenda alipoingia niliweza kumnyooshea mkono wangu aliokuwa umekatwa, lakini hakuonyesha kuwa na huruma na badala yake alinimalizia na panga lingine kwenye mkono huo huo, akazidi kusema.
Akasema kama sio mtu mmoja kujitokeza ambaye yeye hamfahamu, wote wangekuwa maiti ndani ya kibanda hicho, kwa kuwa mtu huyo aliwatuliza wapiga debe hao na kutaka warejee kwenye kazi yao na hivyo kuwapa nafasi wasamaria wema kumuondoa ndani ya kibanda hicho hadi katika kituo cha Afya cha Mwenge na hatimaye kufikishwa Muhimbili na kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa kwamba mtu huyo alifikishwa hapo majira ya saa 6:00 usiku akiwa taabani na haraka alikimbizwa wodini na kupatiwa kitanda.
|