26 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Bibi aliyetelekezwa na wajukuu aomba msaada...hana chakula wala makazi
 
2005-07-26 15:45:44
Na Martha Colman, Mbezi

Bibi mmoja ambaye ana matatatizo ya miguu, aliyejitambulisha kwa jina la Swaumu Ramadhani , 60, mkazi wa Mbezi Luisi, Jijini, anaishi kwa taabu kubwa kutokana na kutokuwa na nyumba ya kuishi.

Bibi huyo ambaye anatembelea magongo, amesema hali yake inazidi kuwa mbaya siku hadi siku kutokana na kutokuwa na pesa ya chakula wala nguvu za kuhangaika kutafuta riziki kwa kulima vibarua.
Amesema ulemavu huo aliupata baada ya kugongwa na baiskeli.

Mbaya zaidi anasema hivi sasa anaishi na wajukuu zake wawili ambao wazazi wao hawana mbele wala nyuma.

’’Niliwachukua wakati nikiwa mzima ambapo nilikuwa naweza kulima vibarua...lakini hivi sasa sina jinsi ya kuwahudumia,’’ akasema.

Amesema kuwa anaishi kwa kutegemea misaada ya watu wanaopita na kumwonea huruma kutokana na hali yake.

Wajukuu hao mmoja ana umri wa miaka mitano na mwingine miaka minne.
Amesema kijana aliyemgonga mpaka leo hamfahamu kwa kuwa ilikuwa ni mida ya jioni na baada ya kumgonga hakusimama kumpa msaada wowote ule.

’’Nilikwenda hospitali ya Serikali Mbezi na kupata matibabu na kuambiwa mguu umevunjika kwa ndani na wakanishauri nikatafute hela ili niende Muhimbili nikafanyiwe operesheni,’’ akasema.

Hata hivyo amesema kutokana na hali yake hakuweza kwenda Muhimbili kuonana na madokta zaidi ya kukaa tu nyumbani na kusubiri kuomba msaada huku na kule bila mafanikio yoyote yale mpaka leo .

’’Mimi naishi kwenye shamba la mtu tu, nilijengewa nyumba ya nyasi na kijana mmoja anayetambulika kwa jina la Sefu, baada ya kunikuta nahangaika mtaani bila kufahamu pa kwenda baada ya kutoka kijijini kwetu Dodoma,’’ akasema.

Amesema binti yake alimtoroka na kumwachia watoto ambao hajui atawalisha nini.
’’Baba wa watoto hawa simfahamu na hapa mjini sina ndugu yeyote...naomba msaada ndugu zangu,’’ akaomba.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.