26 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nauli kwenda Lindi, Mtwara yapanda
 
2005-07-26 15:46:19
Na Abdul Mitumba, Jijini

Watu wanaotumia usafiri wa mabasi kati ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Lindi na Mtwara, wamejikuta wakisaga meno kufuatia ongezeko kubwa la nauli, ambapo sasa wanalipa kati ya Shilingi 15,000 hadi 26,000 kuifikia miji mikuu na wilaya za mikoa hiyo.

Nauli kubwa kuliko zote ni ile inayotozwa na mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Liwale, ambapo abiria mmoja analazimika kulipa Sh.26,000 wakati wale wanaokwenda Newala wanalipa Sh.22,000.

Viwango hivyo vya nauli vimeanza kulalamikiwa na wasafiri, wakidai kuwa ni vikubwa kuwahi kutozwa ukilinganisha na vya mwaka jana wakati kama huu.

Bi.Zainabu Swedi mkazi wa Wazo amesema amelazimika kuahirisha safari yake ya kwenda Liwale kutokana na nauli kuwa kubwa.

Mtu mwingine aliyelilia ongezeko hilo ni Bw.Shaibu Mpende, ambaye alisema nauli ya sh.19,500 ya kwenda mji mdogo wa Ruangwa mkoani Lindi ni kubwa na asingeweza kwenda pamoja na familia yake.

Kufuatia malalamiko hayo, Alasiri ililazimika kuzunguka katika ofisi za makampuni ya mabasi yanayosafirisha abiria kwenda mikoa hiyo, ambapo wote walikiri kuwepo kwa ongezeko hilo la nauli wakisema limetokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Mmoja wa wakatisha tiketi katika kampuni ya mabasi ya Bon Coast, Bi. Hidaya Mnunduma alisema kwa sasa viwango vya nauli kutoka Dar-Lindi ni kati ya Sh.16,000, Dar-Mtwara Sh.18,000, Dar-Masasi hadi Nachingwea Sh.20,000 wakati Dar-Newala ni Sh.22,000 na Dar-Liwale ni Sh.26,000.

Alisema mwaka jana wakati kama huu nauli ilikuwa ni Dar-Lindi Sh.11,000, Dar-Mtwara Sh.14,000, Dar-Masasi hadi Nachingwea Sh.16,000, Dar-Newala Sh.18,000 na Dar-Liwale Sh.20,000.
Akizungumzia ongezeko hilo, Dk.Joyce Rweshobora kutoka Wizara ya Fedha kitengo cha kudhibiti mfumuko wa bei, amesema hali hiyo inatokana na kuanguka kwa shilingi ya Tanzania, hivyo kuruhusu dola ya Marekani kupanda.

Mchumi mwingine Bw.Theo Mushi.
naye ameunga mkono kauli hiyo na kusema matatizo kama hayo yanatokana na kuanguka kwa thamani ya shilingi yetu.

Akasema wafanyabiashara wa magari na mitambo mingine, wamejikuta wakinunua vipuli kwa bei ya juu, hivyo kulazimika kuongeza bei kwa wadau.

Kadhalika Bw.Mushi amesema upandaji huo wa nauli pia unatokana na ongezeko kubwa la mafuta ya kuendeshea magari, ambapo hivi sasa lita moja ya dizeli inauzwa kati ya Sh.900 hadi 1000 kwa lita, wakati petroli inauzwa kati ya Sh.1000 na Sh.1018, kwa lita, wakati mwaka jana wakati kama huu bei ilikuwa kati ya Sh.750 na 850.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.