26 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Rais Karume ataka vyama kukubali matokeo ya uchaguzi
 
2005-07-26 15:47:13
Na Mwinyi Sadallah, Mbweni

Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume amevitaka vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi mkuu kuheshimu matokeo ya uchaguzi.

Akifunga mkutano wa makatibu wakuu wa vyama 18 vya siasa vilivyosajiliwa nchini akasema kwamba kitendo cha kukataa matokeo kinaweza kusababisha migogoro itakayoathiri uchumi na maendeleo ya nchi.

Akasema kwamba kukubali matokeo ya uchaguzi ni njia pekee itakayosaidia kuepukana na matatizo ya kisiasa kama yalivyojitokeza katika chaguzi za nyuma.

’’Tukubali matokeo ya uchaguzi kama yatavyotangazwa na tume zinazohusika na uchaguzi nchini,’’ akasema katika mkutano huo ambao ulifunguliwa na rais wa Tanzania Bw. Benjamini Mkapa.

Bw.Karume akavitaka vyama vya siasa vijitahidi kufanya uchaguzi wa kistaarabu pamoja na kampeni tulivu na kupiga kura kwa utaratibu wa nidhamu uliowekwa.

Akasema kwamba siasa za jazba na chuki ziepukwe hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu wa tatu wa vyama vingi.

Aidha rais huyo akasema kuwa kuna haja ya wananchi kujenga utamaduni wa kutatua migogoro inayozuka nchini kwa njia ya mazungumzo badala ya kutegemea vyombo vya nchi za kigeni.

Awali, mkutano huo uliunda kamati ya muda ya watu saba kupanga utaratibu wa kuvishirikisha vyama vingine katika muafaka wa CCM/CUF uliotiwa saini Oktoba 10,2001 ili kumaliza mgogoro uliozuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Kamati hiyo ambayo imepewa wiki tatu kukamilisha ripoti yake, itakuwa chini ya mwenyekiti wake Bw. Philip Mangula ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM. Mkutano huo ulimchagua Bw. Abdall Nassor kutoka UPDP kuwa katibu wa kamati hiyo.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Bw. Seif Shariff Hamad (CUF), Bimkubwa Mohammed (FORD), Bw Charles Lubala (TADEA), Bw Jacob Nkomola (Sauti ya Umma) na Bw Policia Mwaiseja (NCCR-MAGEUZI).

Kamati hiyo ya muda imepewa hadidu za rejea kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kuandaa muundo wa kamati ya kudumu itakayovishirikisha vyama vyote katika muafaka wa CCM/CUF na kazi za kamati ya kudumu.

Aidha, hadidu rejea nyingine ni kuandaa njia za kuweza kupata fedha za matumizi ya kamati ya kudumu, kuweka maadili yatakayopaswa kuzingatiwa na vyama, utendaji wa kazi zake na namna gani Serikali itaweza kusaidia vyama kifedha hasa vile vidogo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.