|
Binti aomba msaada afanyiwe upasuaji KCMC
2005-07-26 15:48:12
Na Haji Mbaruku, Jijini
Binti mmoja, Beth Ernest Ongombe, 24, mkazi wa Musoma anahitaji msaada wa shilingi milioni moja na nusu ili akafanyiwe upasuaji wa mikono yote miwili katika hospitali ya KCMC, Moshi.
Beth anasema kwa huzuni kuwa, ugonjwa unaomkabili hakuzaliwa nao, isipokuwa ulitokea ghafla tu maishani mwake baada ya kuanza kushikwa na ugonjwa wa degedege na kumfanya awe anaanguka mara kwa mara.
Anasema ugonjwa huo umekuwa ukimsababishia maumivu makali na kukosa hamu ya kula pamoja na usingizi kwa muda mrefu sasa.
Binti huyo ambaye ni yatima na hapa Jijini amekuja kwa lengo la kuomba msaada, ameongea kuwa mkono wake wa kushoto unahitaji kukatwa ili uwekwe wa bandia na ule wa kulia unahitaji kupasuliwa na kunyooshwa ili uwe sawa.
Ninaweza kuwa mzima endapo tu watu wenye huruma na mimi watanisaidia. anasema msichana huyo ambaye hapa Jijini anahifadhiwa na msamaria mwema mmoja aitwae Esther pale Yombo.
Beth analazimika kutumia vidonge vya usingizi ili kupoza maumivu aliyokuwa nayo katika mikono hiyo na anaomba sana watu wenye uwezo wamuonee huruma ili aweze kutibiwa kwa ukamilifu.
Beth anasema kuwa tangu alipofunguliwa akaunti, bado hajaweza kupata msaada wowote, akiomba wenye uwezo kutokata tamaa na hali aliyonayo.
Beth ameomba watu wenye huruma naye wamsaidie kupitia akaunti ya NMB tawi la Musoma yenye akaunti namba 3032501830 ambako ndiko anakoishi na anatarajia kurudi muda si mrefu.
|