26 Jul 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kikwete:Mafiga matatu ni bomba
 
2005-07-26 15:49:01
Na Margareth Simba, Jijini

Mgombea urais kupitia tiketi ya CCM, Bwana Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ili CCM iweze kushinda na kujinafasi katika madaraka yake hadi ipate ushindi wa mafiga matatu!

Bw. Kikwete amesema hayo jana kwenye hafla fupi ya kumpongeza kuchaguliwa kuwa mgombea wa Urais iliyoandaliwa na Baraza la Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na chama.

Akiwashukuru wazee hao kutoka manispaa zote tatu za Dar es Salaam, Bw. Kikwete amesema anatambua umuhimu wa wazee lakini akawatahadharisha kwamba, ili CCM iweze kujinafasi kwenye madaraka mafiga matatu ni lazima.

’’Lazima hayo lazima yawepo kwa sababu mawili hayainjiki chungu,’’ akasema na kisha akafafanua maana ya kauli yake.

’’Itakuwa raha zaidi kama CCM itachukua nafasi ya udiwani na ubunge kwa asilimia kubwa kisha tukamalizia kushinda kwa kishindo kwenye nafasi ya urais...haya ndiyo mafiga matatu ambayo wazee mnapaswa kuyajua na kuyafanyia kazi kwa nguvu, maarifa na uzoefu mlionao,’’akasema.

Aidha amesema kuwa wazee wana wajibu mkubwa wa kuongoza vijana katika kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kuwaongoza kwenye suala zima la upigaji kura, ili waichague CCM kwa sababu vyama vingine vinatishia kuondoa amani ya taifa iliyopo sasa.

’’Nchi hii inapaswa kuongozwa kwa utaratibu unaotakiwa siyo kila mtu ilimradi anatoka chama cha upinzani ...mwenye kudumisha amani iliyopo ni CCM pekee,”akasema na kisha akahoji, ’’Wengine hawajapata madaraka wanatishia kupiga watu. Wakipata je?’’.

Amewahamasisha wazee kuhakikisha CCM inaendelea kutawala kwa sababu ndiyo chama kinachoweza kudumisha amani.

Katika mkutano huo Katibu wa Baraza la Wazee hao, Mzee Mohamed Mtulia, alisema walifarijika sana baada ya wajumbe kule Dodoma kumchagua Kikwete na kuahidi kushirikiana naye katika kila jambo na hasa pale atakapohitaji msaada wao.

Katika hafla hiyo Bw. Kikwete alisimikwa kwa kupewa kigoda ambacho alizawadiwa na wazee wa Ilala, fimbo kutoka kwa wazee wa Temeke na kitambaa cha rangi ya kijana maarufu kama mgolole alichopewa na wazee wa Kinondoni.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.