|
Kijana ajinyonga
2005-07-26 15:50:22
Na Janneth Kiure, Kibaha
Mwanaume mmoja aitwaye Miraji Shabani, 18, mkazi wa kijiji cha Mwambwito kata ya Ruvu wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani, amekutwa amekufa baada ya kujitundika kwenye mkorosho kwa kutumia kamba ya katani.
Mwili wa mtu huyo umekutwa katikati ya pori la Mwambwito.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani Ally Mbilikira amesema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa moja asubuhi baada ya watu kuuona mwili wa marehemu ukiwa unaninginia juu ya mti wa mkorosho.
Wasamaria hao walipiga mayowe kwa nia ya kuomba msaada na baadaye wakatoa taarifa katika kituo cha Polisi... askari walifika kwenye eneo la tukio na kufanikiwa kuufanyia uchunguzi, akasema Kamanda.
Amesema chanzo cha kijana huyo kukatisha maisha yake hakijajulikana hadi sasa lakini akasema polisi wanaendelea na uchunguzi.
Katika tukio lingine watu wawili wakazi wa eneo la Magomeni wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani wanashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya aina ya bangi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mbilikira, watuhumiwa hao walitiwa mbaroni jana majira ya saa tatu usiku wakati wakiwa katika harakati ya kutafuta wateja wa dawa hizo.
Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Makamba Juma, 32, pamoja na Juma Iddi, 18, wote wakiwa ni wakulima wa wa Magomeni.
Afande Mbilikira amesema watuhumiwa hao walikamatwa na polisi ambao walikuwa wanafanya doria katika eneo hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia kwamba katika eneo la Magomeni wapo wahalifu ambao wanajihusisha na biashara ya kuuza midawa ya kulevya.
Watuhumiwa wote ni wauzaji na watumiaji wa dawa hizo na mara baada ya upelelezi kukamilika wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
|