22 Sep 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Makamba avamiwa na majambazi Dar
 
2005-09-22 16:47:15
Na Mwandishi Wetu, Jijini

Wakati Jeshi la Polisi limeanzisha kampeni kabambe ya kuwashughulikia majambazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yussuf Makamba ameonja joto ya jiwe baada ya nyumba yake kuvamiwa jana usiku na majambazi wapatao saba.

Tukio hilo la aina yake lililotokea majira ya saa mbili usiku, lilikuwa kama sinema au mchezo wa kuigiza, kwani hakuna aliyekuwa akifikiri nyumba ya mzito kama Makamba iliyoko Wazo Hill nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ingeweza kuvamiwa na majambazi ambayo awali yalivurumisha risasi kama njugu.

Majambazi hayo kabla ya kuvamia nyumba ya Mkuu wa Mkoa iliyojengwa karibu na pampu ya kusukumia maji kuelekea katika Kiwanda cha Saruji cha Wazo, ambayo hulindwa masaa 24 na walinzi wa Group 4, yalivamia kiduka kidogo na kumjeruhi kijana mmoja kwa risasi.

Habari hizo zinaendelea kusema kuwa majambazi hayo yaliyokuwa zaidi ya saba, yalipora fedha katika kiduka hicho na kutinga ndani ya nyumba ya Makamba ambako walifanikiwa kupora mabegi ya nguo na vitu vingine ambavyo hata hivyo bado havijajulikana ni vitu gani na thamani yake halisi.

Chanzo hicho cha habari kinasema kuwa majambazi hayo ili kuwatishia majirani wasijitokeze, mara kwa mara yalikuwa yakipiga risasi hewani, kitu ambacho kiliwaweka katika wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo ambao wengine walitimua mbio hivyo wasijue la kufanya.

Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho hata hivyo hakikupenda kabisa kutajwa gazetini, majambazi hayo baada ya kukusanya walichoona kinawafaa walitokomea zao huku wakipiga tena risasi hewani na kuwafanya baadhi ya wakazi wa maeneo hayo, kujifungia zaidi ili wasijekumbwa na mkasa huo.

Hii ni mara ya pili kwa nyumba hiyo ya Makamba kuvamiwa, wakati fulani huko nyuma maeneo hayo yalivamiwa na majambazi na kupora kwenye baa moja maarufu iliyokaribu na nyumba hiyo ya mkuu wa mkoa.

Baadhi ya watu walisikika wakiuliza kwa mshangao ’’inakuwaje hata kwa mzee mwenyewe (Makamba) kunavamiwa na majambazi, hii inatisha sasa, sisi ambao hatuna uwezo wa kulindwa tutafanya nini, Serikali lazima iangalie upya suala la usalama wa raia na mali zao.’’

Mkazi mwingine alisema kuwa polisi lazima waanzishe ’’patrol’’ na wapatiwe zana za kisasa kama magari na hata silaha ili kuweza kupambana vilivyo na hali hii ya ujambazi ambayo sasa imeonekana kupamba moto kila kukicha sio tu Jijini Dar es Salaam, bali hata mikoani.

Kufuatia taarifa hizo, Alasiri ilipowasiliana na Mkuu huyo wa Mkoa, Luteni Yusuf Makamba mwenyewe alisema kwa sasa yuko Songea.

’’Hivi sasa niko Songea ndugu yangu lakini nimepata taarifa ya kuvamiwa nyumbani kwangu. Ila ninachokuomba wasiliana na RPC atakupa maelezo zaidi’’, akasema Makamba ambaye kwa sasa yupo mjini huko kwa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.

Akizungumza nasi mapema asubuhi leo baada ya kutaka ufafanuzi, Kamanda Tibaigana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa majambazi hao pamoja na vitu vingine, walipora pesa taslimu sh.54,000 pamoja na simu ya mkononi ya mmoja wa wapangaji wa mzee Makamba.

Hata hivyo, Kamanda Tibaigana amewataja watu hao kuwa ni vibaka, ambao kulingana na taarifa aliyonayo walivamia nyumba hiyo wakitumia mapanga, marungu na nondo kisha kupora vitu na pesa hizo.

Akafafanua kuwa, katika nyumba hiyo ndogo iliyo ndani ya geti kubwa pamoja ya nyumba kubwa ambayo hata hivyo haijaanza kutumiwa na mzee Makamba, walikuwemo wapangaji wake pamoja na mama yake mzazi mzee Makamba ambaye hakumtaja jina.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.