|
Aomba msaada akatibiwe baada ya kuangushiwa mkongoto
2005-09-26 16:50:25
Na Adam Fungamwango, Temeke
Kijana mmoja mkazi wa Mbezi Beach Jijini, Allan Lusajo Semu 30, amedai kupigwa na mtu mmoja aliyevalia nguo za askari polisi na kumvunja mkono wa kushoto.
Bw.Lusajo amesema tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya Temeke, ambapo alikuwa amekwenda kumuona kumjulia hali mpenzi wake aliyemtaja kwa jina la Joyce.
Amesema wakati anaondoka huku akiwa anasindikizwa na mpenzi wake huyo majira ya saa mbili usiku, waliingia sehemu moja ambayo ni ya kichochoro na giza, ndipo wakakutana na mtu huyo ambaye alikuwa amevalia nguo za kiaskari polisi.
Kwanza alitusimamisha mimi ni mpenzi wangu na kutoa kitambulisho chake akidai kuwa eti yeye ni askari polisi, lakini nikamwambia kuwa huu si usiku na ni giza sitoweza kusoma kitambulisho chako, akasema na kisha kuongeza kuwa mtu huyo alimvamia ghafla na kuanza kunipiga.
Akaendelea kusema kuwa, alipata kipigo cha nguvu hadi kuchaniwa shati na suruali huku mpenzi wake akiwa analia, akishindwa kabisa kumsaidia kutokana na mtu huyo kutumia nguvu nyingi na ukatili wa hali ya juu.
Bw. Lusajo ameongeza kuwa katika sakata hilo, alipoteza pesa kiasi cha Sh.98,250.
Amesema aliokolewa na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi ambaye alimbeba na kumkimbiza moja kwa moja kituo cha polisi cha Temeke Wailes.
Nililala pale hadi asubuhi na baada ya hapo, mlinzi yule alifika na kutoa maelezo yake na mimi pia nikatoa maelezo na baadaye nikafungua jalada la kesi namba WWP/RB/1234/05.
Yeyote anayetaka kumsaidia anaweza kuwasiliana naye kwa simu namba 0745 946165.
|