|
Wahitimu wa shule watakiwa kuzingatia elimu
2005-09-26 16:55:45
Na Mwandishi Wetu, Ukonga
Wanafunzi wametakiwa kuzingatia elimu kwa kuwa ndiyo mkombozi pekee wa maisha yao ya baadaye katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiuchumi na mfumo wa utandawazi.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa shule ya Mtakatifu Theresa ya Ukonga Jijini, Sista Perpetual Muhana wakati wa mahafali ya kwanza ya shule hiyo yaliyofanyika juzi.
Aliwataka wahitimu hao kuhusisha malezi bora waliyoyapata shuleni hapo kwa kipindi cha miaka saba walichokuwepo na yale ya wazazi ili kuendeleza sifa nzuri ya shule hiyo.
Kadhalika aliwataka wazazi kuwasaidia wahitimu hao katika jitihada zao za kujiendeleza kielimu ili hatimaye wafanikishe ndoto zao za kuwa watalaam wazuri na wa kutegemewa na jamii.
Kwa upande mwingine, Serikali imeombwa kwa kupitia mpango wake wa MMEM kuzisaidia shule binafsi ili ziweze kuendeleza na kuboresha kiwango cha elimu kitolewacho kwa wanafunzi.
Kadhalika imeombwa kuandaa mtiririko mzuri wa vitabu vya kiada kwa ajili ya shule binafsi zinazotoa mafunzo yake kwa lugha ya Kiingereza.
Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 14 walihitimu na kukabidhiwa vyeti vyao. Pia walipewa zawadi kadhaa kutokana na kungara katika masomo, nidhamu, mahudhurio na mambo mengine.
Awali wanafunzi wa shule hiyo walichengua wageni kutokana na umahiri wao katika kuendesha Bunge la Watoto ambapo walijadili mambo kadhaa ya kielimu na kijamii yanayowagusa moja kwa moja.
Pia wanafunzi hao walifanya maonyesho ya kitaaluma ambapo walionyesha umahiri wao katika kufanya majaribio ya Kisayansi kama upasuaji wa wanyama.
Kadhalika wanafunzi hao walifanya jaribio juu ya kusinyaa na kupanuka kwa maada, utambuzi wa aina ya chakula kwa kutumia madawa, jinsi ya kumtambua mgonjwa wa kisukari kwa kupima mkojo, kupima uzito na maada tofauti pamoja na kupima kiasi cha umeme kwa kutumia kipima umeme.
Kwa upande wa michezo, wanafunzi hao walionyesha umahiri wao katika kuimba, kucheza ngoma za asili, sarakasi, jaiving na kuimba mashairi.
Shule ya Mtakatifu Theresa ilianza Januari 9 mwaka 1999 ikiwa na watoto 120 na walimu watano.
Mahafali hayo ni ya kwanza tangu kuanzishwa kwa shule hiyo inayomilikiwa na Masista wa Kikatoriki wa Shirika la Mtakatifu Theresa.
Licha ya shule hiyo, shirika hilo linaendesha shule ya Nyakahoja ya mjini Mwanza pamoja na Hekima Girls ya mkoani Kagera.
|