|
Wazazi waaswa kutoozesha watoto wao wa kike mapema
2005-09-27 14:02:33
Na Yasmine Protace, Mkuranga
Wazazi wameshauriwa kutowaozesha watoto wao wa kike, pale wamalizapo elimu ya msingi na badala yake kuwaendeleza kwa masomo ya sekondari.
Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kilimahewa, Mkuranga, Bw.Mkenda A.Mkenda wakati wa mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo, yaliyofanyika shuleni hapo.
Bw.Mkenda amewaambia wazazi kuwa watoto wa kike wamalizapo elimu ya msingi wanatakiwa kuendelea na sekondari kwani kuwaozesha inakuwa si kuwatendea haki.
Inafaa kila mtoto wa kike akimaliza shule, apatiwe elimu ya sekondari na sio kumuozesha kwani elimu ya msingi haitoshi,akasema.
Amesema huu mchezo upo sana vijijini ambapo baadhi ya wazazi wakiona mtoto amemaliza tu masomo ya msingi wanampa ruksa ya kuolewa.
Licha ya tatizo hilo, amesema shule hiyo pia inakabiliwa na ukosefu wa meza za walimu, vyumba vya madarasa na maji.
Naye Mkuu wa Shule ya sekondari ya St.Mathews Bw.. Hassan Lucas, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkurugenzi wa shule hizo, Bw. Thadeo Mutembei, amekubali kuwa mlezi wa shule hiyo kutokana na walimu kumuomba.
Amesema amekubali kuwa mlezi na hivyo atashirikiana na walimu wa shule hiyo ili kuhakikisha anawasaidia kwa chochote alichonacho ili kuhakikisha shule inakuwa na mwelekeo mzuri wa ufundishaji na wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Pamoja na kukubali kuwa mlezi, Bw. Mutembei ameichangia shule hiyo
Sh.laki moja na nusu, ili pesa hizo ziweze kuwasaidia walimu na wanafunzi katika kutatua matatizo ya shule.
Kwa upande wa kijana wa kijiji hicho ambaye wazazi wake wamefariki na kumfanya yeye kuishia kidato cha pili kwa kukosa ada, amekubali kumsomesha mpaka Chuo Kikuu endapo atajitahidi katika mitihani yake ambayo atakuwa anaifanya.
Jumla ya wanafunzi 83 walihitimu elimu ya msingi.
Mahafali ya shule hiyo yalipambwa kwa nyimbo za kizazi kipya zilizoimbwa na vijana hao kwa umahiri wa hali ya juu.
|