|
Chama cha umoja wa wazee chaomba msaada
2005-09-27 14:03:23
Na Francisca Jeremiah, Ubungo
Chama cha Umoja wa Wazee Kinondoni kinachojishughulisha na usafi wa mazingira kwa kuzoa taka, kimeomba msaada wa vifaa mbalimbali vya kuwawezesha kufanyia usafi.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili katika ofisi za chama hicho zilizopo Ubungo Riverside, mwenyekiti wa chama hicho Bw. Ally Mwinyimkuu, amesema kwa sasa chama hicho kina uhaba wa vitendea kazi, hali inayokifanya kishindwe kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Bw. Mwinyimkuu, chama hakina msaada na kuwa wamekuwa wakichanga pesa zao na kununua vifaa ambavyo bado haviwezi kutosheleza kwa maeneo ambayo wanayafanyia usafi.
Aidha akasema kuwa chama hicho kina wanachama 21 ambapo wanachama wake wote ni wazee ambao wameshastaafu na wameamua kuunda chama ili waweze kujishughulisha.
Vifaa vinavyotakiwa ni pamoja na gari la kupelekea taka dampo,mifagio pamoja na vifaa vingine ya kuzolea taka.
Hata hivyo Naibu Kaimu wa chama hicho Bw. Azizi Mpururu amesema licha ya kuwa na vitendea kazi duni, wanachama hao wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi zao vizuri.
Amesema kitu kinachowakwamisha zaidi ni wakazi wa eneo hilo kutokuwa na elimu ya usafi na hivyo kuwa wagumu kulipa ushuru wa taka pale wanapokuwa wamesafishiwa maeneo yao .
Wakazi wa eneo hili hawapendi kulipa ushuru matokeo yake huvizia usiku na kutupa taka barabarani.
|