|
Wakazi wa Lindi waishio Jijini wachanga mamilioni
2005-09-27 14:04:09
Na Abdul Mitumba, Mburahati
Wakazi wa kata ya Kitomanga katika jimbo la uchaguzi la Mchinga wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi wanaoishi Jijini Dar es Salaam, wamekusanya shilingi milioni 5.6 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa shule ya sekondari.
Jumla ya shilingi milioni 44.5 zinahitajika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ya kata.
Kati ya hizo, Sh.640,730 zimepatikana kwa kuwashirikisha wakazi wa kata hiyo kupitia makato ya kiasi cha pesa kinachokatwa kutoka kila kilo moja ya zao la ufuta linalolimwa katani humo.
Mchango huo kwa wakazi wa kata ni hatua ya awali iliyoanza Septemba mwaka jana ambapo wahusika wakuu ni vijiji, kaya na chama cha ushirika cha kata hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Kamati ya ujenzi wa shule hiyo, Bw.Masoud Msagula katika mkutano wa wana kamati uliofanyika katika majengo ya Shule ya Msingi Mburahati, jijini Dar es Salaam.
Alisema lengo la kamati yake ni kuhakikisha madarasa manne yanajengwa katika kipindi cha mwaka 2004/05, jingo la utawala ifikapo mwakani na pia nyumba mbili za walimu ziwe zimekamilika hadi kufikapo mwaka 2007.
Bw.Msagula amesema hatua ya kujenga shule hiyo inafuatia watoto wengi wanaofaulu kushindwa kupata nafasi ya kuingia sekondari na kutoa takwimu kuwa liha ya watoto 92 kufaulu kati ya mwaka 2002 na 2004 ni 67 tu ndiyo waliopata nafasi.
|