27 Sep 2005 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wastaafu ondokeni Jijini dar, Vibaka wanakula ’taimingi’ kuwapora mafao
 
2005-09-27 14:07:31
Na Simon Mhina, Jijini

Ama kweli Ngo’mbe wa masikini hazai, na akizaa Ndama hufa! Maneno hayo ya wahenga yametimia kwa mstaafu moja wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo baada ya kulipwa mafao yake vibaka wakampora kitita chote na kumwacha mikono mitupu!

Uchunguzi wa Alasiri umeonyesha kuwa bado kuna wastaafu ambao hawajalijua jiji.

Wastaafu wengi wameonekana wakirandaranda jijini Dar kuangalia vitu madukani bila kujua kuwa vibaka wanawalia ’taimingi’ ya kuwapora.

’Wastaafu, tafadhali ondokeni jijini, hawa vibaka watawaliza. Wanawafuata kila kona’, Bw. Melkiori Mosha wa Buguruni Malapa amewaonya wastaafu.

Amesema kuwa wastaafu hao hata wakipita jijini wanatambulika bila mtu kupewa ’introduction’.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Jeshi hilo Kamishina msaidizi mwandamizi wa Aden Mwamunyange, baada ya mstaafu kuchukua kitita chake, vibaka wakamlia taimingi na dili lao likaliki.

Hata hivyo, akizungumza kwa njia ya simu Mwamunyange alikataa katakata kutaja jina la mzee huyo wala eneo analotoka kwa kile alichosema ni uchaguzi mkali unaofanyika.

’Nimelazimika kwanza kutoa tahadhari, kwa vile walio wengi badi wangali wanachukua mafao yao, habari ya jina na mahali tulieni kwanza uchunguzi unafanyika,’akasema.

Habari zinasema huenda dili la kumpora mzee huyo, lilianza kusukwa na vibaka tangu akiwa nyumbani, na pengine ndio maana vijana wa Mahita, hawataki kumtaja jina wala eneo.

Mwandishi mmoja alionekana kuguswa na tukio hilo mara baada ya taarifa ya Mwamunyange kupokelewa pale Maelezo, akasema kuporwa kwa mstaafu huyo ni dhambi kuu ya kufunga mwaka huu.

’Mimi hivi sasa nina watoto wakubwa tu, lakini tangu nizaliwe, hadi utoto wangu na sasa utu uzima nilikuwa nasikia kilio cha wafanyakazi wa Afrika mashariki, leo huyu amelipwa anaporwa!’ akasema kwa huzuni.

Awali katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jeshi la Polisi nchini limewaonya wazee, wastaafu hao, kuwa waangalifu na vibaka wanaowafuatilia, baada ya kulipwa mafao yao benki.

Taarifa hiyo ya kurasa mbili imewaonya waastaafu hao, kutochukua kiasi kikubwa cha fedha.

Ikasema tayari kuna taarifa kwamba mstaafu mmoja ameporwa na vibaka pesa zake, mara tu baada ya kulipwa.

’Jeshi la polisi limelazimika kutoa tahadhari hiyo baada ya mstaafu mmoja kuporwa fedha zake zote na vibaka hao, ambao walikuwa wakimfuatilia kwa makini na kufanikiwa kuchukua fedha zake,’ikasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo, imesema Jeshi la polisi linawashauri wastaafu hao wafuate maagizo ya wizara ya fedha kwamba wachukue fedha kidogo au wakubali fedha zao zihifadhiwe kwenye akaunti zao.

Ikasema wakifanya hivyo, itawabidi wachukie fedha zao kidogo kidogo kwa kadri ya mahitaji yao, na hivyo kuepuka kuporwa na vibaka ambao huwafuatilia.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.